WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Waislamu watumie nyumba za ibada kuhubiri uislamu na misingi yake.
Ametoa wito huo jana mchana (Ijumaa, Oktoba 28, 2016) wakati akishiriki sala ya Ijumaa katika msikiti wa Nunge mjini Dodoma.
Alisema
dini ya Kiislam inafundisha kwamba sala ndiyo msingi mkubwa unaopaswa
kufuatwa na kila muumini hivyo ni lazima wafanye ibada kwa wakati.
“Nasisitiza
kwamba wote tutumie muda wetu vizuri pamoja na mambo mengine tufanye
ibada kwani dini inatuekeza kuwa sala ndiyo msingi mkubwa kwenye
Uislamu. Tunayo kazi ya kuimarisha misingi ya dini kwa kutumia nyumba za
ibada,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema Waislamu wana jukumu la kufundisha watoto wao na
kuhakikisha wanakua kwenye imani na kujengeka katika maadili mema.
“Dini
inajenga maadili mema kwa mtoto na hata mtu mzima. Pia dini inajenga
misingi ya uvumilivu na inamuwezesha mtu kumtambua Mwenyezi Mungu.
“Tuendelee kuwafundisha vijana wetu umuhimu wa kushiriki kikamilifu
kwenye masuala ya kidini ili wakikua waweze kuiendeleza kwa vizazi
vijavyo,” alisema.
Waziri
Mkuu ambaye alitumia fursa hiyo kujitambulisha kwa waumini wenzake wa
mkoa wa Dodoma baada kuhamia rasmi, ameahidi kutoa ushirikiano kwao na
pia amewaomba wampe ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake
ipasavyo.
“Nimekuja
kujitambulisha. Mimi ni kijana wenu, ndugu yenu. Nimekuja Dodoma rasmi
nyumbani na kikazi. Naomba mnipokee na naamini katika kipindi chote
nitakachokuwa hapa nitapata ushirikiano nanyi na pia nitawapa
ushirikiano,” alisema.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu aliwaomba waumini hao wawaombee dua
wanafunzi wa kidato cha nne ambao wanatarajia kuanza mitihani ya
kuhitimu Novemba Mosi, mwaka huu ili waweze kufaulu.
Waziri
Mkuu aliwaomba waumini hao waendelea kuwaombea viongozi wa kitaifa
wakiongozwa na Rais Dk. John Magufuli ili waweze kutekeleza vizuri
majukumu yao na kufikia malengo yanayotarajiwa na wananchi.
Aidha,
Waziri Mkuu alichangia sh. milioni moja kwa ajili ya kuendeleza mradi
wa ujenzi wa zahanati katika msikiti huo. Miradi inayojengwa na waumini
wa msikiti huo kwa sasa ni zahanati, madarasa ya shule ya awali na shule
ya ufundi.