Benki
Kuu ya Tanzania imetangaza rasmi kuchukua usimamizi wa Benki ya Twiga
Bancorp kuanzia jana kutokana na upungufu wa mtaji wa benki hiyo kiasi
cha kuwa na deni la Shilingi Bilioni 21.
Benki
Kuu pia imesimamisha shughuli zote za utoaji huduma za kibenki za benki
hiyo kwa kipindi kinachokadiriwa kufikia wiki moja kuanzia jana tarehe
28/10/2016 ili kutoa nafasi kwa ajili ya kupanga taratibu za uendeshaji
wa benki hiyo.
Maamuzi
hayo yametangazwa jana jijini Dar es Salaam na Gavana wa Benki Kuu,
Prof. Benno Ndullu mbele ya waandishi wa habari, na kusema kuwa hatua
hiyo ni kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 56 (1)(g)(i) na 56(2) a-d
cha taasisi za fedha ya mwaka 2006.
"Uamuzi
huu umechukuliwa baada ya kubaini kuwa benki ya Twiga ina upungufu
mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya mabenki na Taasisi za
Fedha ya Mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu wa mtaji unahatarisha
usalama wa sekta ya fedha na pia kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa
benki ya Twiga kutaharisha usalama wa amana za wateja" Imesema sehemu ya taarifa ya Prof. Benno Ndullu.
Aidha,
amewataka watu wote wanaodaiwa na benki hiyo kulipa madeni yao kupitia
Benki Kuu ya Tanzania, na kwamba wadaiwa wote watafuatiliwa kokote
waliko.
Mbali
na maamuzi hayo, benki hiyo pia imeisimamisha Bodi ya Wakurugenzi na
uongozi wa benki hiyo, huku ikimteua Meneja Msimamizi ambaye atakuwa na
jukumu la kusimamia shughuli za benki hiyo kwa kipindi ambacho itakuwa
chini ya usimamizi wa benki hiyo.
Kwa
upande wake mkurugenzi wa usimamizi wa mabenki Bw. Keddedy Nyoni
amesema benki hiyo ilianza na mtaji wa bilioni 7.5 lakini sasa ina deni
la hadi bilioni 21.