Na Ally Daud-Maelezo
MADAWA
bandia na yasiyo sahihi kwa matumizi ya binadamu yamekamatwa maeneo ya
Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini baada ya kufanyika ukaguzi maalum
wa kutafuta dawa bandia katika maeneo hayo iliyofanyika hivi karibuni.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw.
Hiiti Sillo wakati wa kutoa Matokeo ya ukaguzi maalum wa dawa
uliofanyika katika mikoa ya Kanda za Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.
“Kutokana
na ukaguzi maalum tulioufanya katika Kanda za Ziwa pamoja na Nyanda za
Juu Kusini wa kutafuta dawa bandia na zisizo sahihi kwa matumizi ya
binadamu tumefanikiwa kukamata dawa bandia za aina tano ambazo zipo
kwenye makundi mawili ya Dawa za malaria na Viua vijasumu(Antibiotics)” alisema Bw. Sillo.
Aidha
Bw. Sillo amesema kuwa ukaguzi huo maalum umeweza kusaidia kukamata
dawa ya malaria aina ya vidonge vya Quinine ambayo inadaiwa kutengenezwa
katika kiwanda cha Elys Chemical nchini Kenya na nyingine
zinatengenezwa hapa nchini katika kiwanda cha Shelys Phamaceuticals Ltd.
Mbali
na hayo Bw. Sillo amesema kuwa pamoja na kukamata dawa bandia pia zoezi
hilo lilifanikiwa kubaini na kukamata dawa zilizoisha muda wa matumizi ,
zisizosajiliwa na zenye ubora duni zenye thamani ya Tsh. Milioni
17.463.
Bw.
Sillo ameongeza kuwa Ukaguzi huo ulitokana na kuwa na taarifa za awali
ambazo zilionyesha uwepo wa dawa bandia katika maeneo ya Geita na Mara
mwezi Agosti na Septemba mwaka huu na kusistiza kwamba zoezi hilo la
ukaguzi linaendelea nchini kote na watakaokutwa na hatia watachukuliwa
hatua stahiki.
Kwa
upande wa Msajili wa Baraza la famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe amesema
kuwa wataalamu wa madawa watakaokutwa na hatia ya kusambaza na
kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili na kuacha kutoa huduma kwa
mujibu wa sheria ya dawa , chakula na vipodozi.
“Wataalamu
wa dawa ambao wanasambaza na kuhudumia dawa bandia watafutiwa usajili
na kuacha kutoa huduma kwa mujibu wa sheria ya dawa , chakula na
vipodozi pindi watapogundulika” alisema Bi. Shekalaghe.
Zoezi
hilo la Ukaguzi maalum wa dawa bandia ulianza Oktoba 4 mwaka huu
linafanywa kwa ushirikiano wa TFDA, Jeshi la polisi pamoja na Maafisa
kutoka Baraza la Famasi litakuwa endelevu ili kuhakikisha dawa bandia
zinatoweka nchini.