WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey
Zambi kuhakikisha anadhibiti wafanyabiashara wanaonunua korosho kwa njia
ya magendo na atakayekamatwa achukuliwe hatua.
Pia
amewataka wananchi wa mkoa huo kutouza korosho zao kwa walanguzi
maarufu kangomba na badala yake wazipeleke kwenye masoko rasmi ili
waweze kupata tija.
“Biashara
ya kangomba ni mwiko atakayekamatwa amebeba korosho za kangomba
atachukuliwa hatua za kisheria na chombo chake cha usafiri
kitataifishwa” alisema.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo jana Jumatatu, Oktoba 17, 2016 wakati
akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa wilaya ya Ruangwa katika
mikutano iliyofanyika kwenye vijiji vya Mibure, Namakuku, Ng’imbwa,
Chienjele, Mkata, Mitope na Kitandi
“Marufuku
kuuza korosho kwa kangomba kwani mnapata hasara kipimo kinachotumika si
rasmi. Mkoa kamateni na taifisheni korosho na chombo cha usafiri
kitakachotumika kubeba korosho za magendo,” alisema.
Alisema
ni vema wakulima wakaachana na biashara ya kangomba kwa sababu haina
tija na badala yake wasubiri na kwenda kuuza korosho zao katika minada
kwa bei nzuri.
“Mwaka
huu korosho itauzika kwa bei ya juu zaidi isiyopungua sh.3500,
msikubali kuuza korosho mlizizitolea jasho kwa walanguzi wanaotumia
kangomba kwa sh. 1000 huu ni wizi, kwani kile kipimo cha wanachotumia ni
sawa na kilo mbili, hivyo unapoteza zaidi ya sh. 6000”. alisema
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu aliwasisitiza wananchi hao kuongeza idadi ya
mazao ya biashara na kuanza kulima alizeti ambapo wataweza kupata faida
ya zaidi ya sh. milioni moja kwenye shamba la ukubwa wa ekari moja.
Wakati
huo huo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi ametoa miezi miwili
kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea
Chezue kuhakikisha ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mibure unakamilika.
“Ndani ya miezi miwili Zahanati iwe imekamilika, tuache kuzungumza sasa
ni vitendo tu”amesema.
Awali
Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kukamua mafuta ya ufuta na karanga
cha Ilulu kilichoko wilayani Nachingwea na kukuta kimetelekezwa.
Aliagiza
uongozi wa kiwanda kumpelekea nyaraka zote za umiliki. Kiwanda hicho
kilibinafsishwa kwa marehemu Abbas Gulamali na sasa kinasimamiwa na
familia yake.
“Nawahitaji Dodoma Oktoba 22 waje na nyaraka zao ili nijue walipokabidhiwa kiwanda hiki walitaka kufanya nini,” alimuagiza Msimamizi wa Kiwanda hicho Dinna Mavumbi kuwajulisha wahusika.
Waziri Mkuu alisema haiwezekani kiwanda hicho kilichojengwa kwa fedha za umma kikatelekezwa bila ya kuendelezwa.
Alisema
baada ya kupitia nyaraka zao ataangalia namna ya kurudisha majengo hayo
ya kiwanda kwa Serikali. “Hatuwezi kuacha raslimali hii ikiwa
imetelekezwa msituni inaharibika.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, OKTOBA 17, 2016
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa na Mkewe Mary Majaliwa wakiangalia kiwanda cha
ILULU kilichokuwa kinatengeneza mafuta ambacho muekezaji amekifanya kuwa
Ghala nakukitelekeza na watu kuiba vifaa na kufanya uharibifu mkubwa
.Kiwanda hicho kipo wilaya ya Rungwe Mkoani Lindi .Waziri Mkuu yupo
katika ziara ya kikazi katika wilaya ya Nachingwea na Rungwe Mkoani
Lindi(Picha na Chris Mfinanga)