test

Jumamosi, 15 Oktoba 2016

CHADEMA: Kuhusu uamuzi wa Rais Magufuli katika kuhitimisha mbio za mwenge


CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

KUHUSU

UAMUZI WA RAIS MAGUFULI KATIKA KUHITIMISHA MBIO ZA MWENGE 

Rais Dk. John Magufuli kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ametoa tamko la kuwazuia watendaji wa ngazi mbalimbali za Serikali wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Mamaya na Wenyeviti wa Halmashauri kutohudhuria sherehe za uzimwaji wa Mwenge Wa Uhuru zilizopangwa kufanyika Bariadi, Mkoo wa Simiyu Ijumaa Oktoba 14, 2016 na kwa wale ambao walikwishalipwa posho za safari wazirejeshe.


Aidha, taarifa hiyo ya Ikulu ilielezea kuwa Rais Dk. Magufuli atawakilishwa katika hafla hiyo na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.

Kitendo cha Rais Dk. John Pombe Magufuli cha kumteua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohammed Shein kumwakilisha katika hafla ya kilele cha kuhitimisha Mbio za Mwenge kitaifa Bariadi, Mkoani Simiyu huku upande wa pili akiwakataza viongozi waandamizi wa serikali yake wakiwemo Mawaziri na Wakuu wa Mikoa kutohudhuria sherehe hizo, kimedhihirisha hoja mbili muhimu;

1. Uhalali na uchaguzi wa marudio wa Zanzibar na hadhi ya kisiasa ya Rais Shein

2. Uhalali wa kuendelea na mbio za Mwenge

Kutokana masuala hayo mawili, chama kinapenda kutoa kauli ifuatayo;
Uamuzi wa Rais John Magufuli kumwondolea itifaki ya kitaifa mtu ambaye ameapishwa Kikatiba na Kisheria kuwa Rais wa Nchi, unasaidia kuendeleza mjadala mzito kuhoji kuhusu uhalali wa uchaguzi wa marudio wa Zanzibar uliotumika kumpatia ushindi Rais Shein ambao kama ambavyo imeshaelezwa kwa kina, kuwa ulilazimishwa kufanyika kwa matakwa ya CCM, huku misingi ya Katiba na Sheria za nchi zikivunjwa.

Kama Serikali ya CCM, chini ya Rais Magufuli wangekuwa wanatambua kuwa Uchaguzi uliomweka madarakani Rais Shein ulikuwa halali, huru na haki, hivyo kumpatia uhalali wa kisiasa kushikilia nafasi hiyo aliyonayo, serikali isingefanya uamuzi wa kumwondolea itifaki zote za kitaifa katika sherehe hiyo ambazo zinaendana na nafasi yake. 

Viongozi waandamizi wa kiserikali waliozuiliwa kuhudhuria, kumsindikiza na kumpokea Rais Shein katika tukio hilo wakiwemo Mawaziri, ndiyo wanaounda itifaki ambayo ingemstahili Rais Magufuli iwapo angeamua kushiriki yeye mwenyewe kama mgeni rasmi. 

Aidha hatua hiyo ya kumuacha Rais Shein apokelewe na kusindikizwa na viongozi wa Mkoa wa Simiyu mwendelezo wa kuwadharau Wazanzibar, kuidharau Nchi ya Zanzibar na hata kumshushia hadhi kiongozi huyo na kuhalalisha mjadala wa uhalali wa urais wake kisiasa. 

Kutokana na hatua hiyo ambayo ni wazi imewashatua wengi, litakuwa jambo la busara iwapo Rais Magufuli akaweka wazi iwapo msimamo wake kuhusu uhalali wa Uchaguzi wa Marudio wa Zanzibar umebadilika na sasa amebaini ukweli katika hoja za Watanzania wanaohoji kuhusu uchaguzi huo uliolazimishwa kinyume na Katiba na Sheria za Nchi. 
Vinginevyo kwanini, iwapo Rais Shein alipatikana kihalali na anatambulika kihalali kama Rais wa Zanzibar, asipewe heshima yake inayostahili anaposhiriki matukio ya kitaifa Tanzania Bara ama anapotumika katika matukio kama ilivyo katika tukio la uzimaji Mwenge.

Hata hivyo, kutoshiriki kwake Rais Magufuli na kuzuia viongozi wa waandamizi wa Serikali yake kutoshiriki na kumuacha Rais Dk Shein na viongozi wa Mkoa wa Simiyu pekee, inathibitisha msimamo wa muda mrefu ya CHADEMA kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru hazina tija yoyote na kuwa zinatakiwa kusitishwa, fedha zinazotumika ziokolewe na kuelekezwa katika matumizi mengine muhimu kwa wananchi na Mwenge uhifadhiwe makumbusho ya taifa. 

Hatushawishiki hata kidogo kuamini kwamba uamuzi wa Dk Magufuli wa kuzuia viongzi waandamizi kutoshiriki hafla hiyo ya kitaifa kuwa inalenga kubana matumizi ya serikali kwani tayari Serikali hiyo hiyo ya Rais Magufuli ndiyo iliyopanga na kuidhinisha matumizi makubwa ya mabilioni ya fedha kutumika kuukimbiza Mwenge huo nchi nzima.

Aidha, kama angekuwa na dhamira njema na fedha za walipa kodi wa nchi hii, angezuia gharama hizo kwa kuzuia mbio za Mwenge ambao kimsingi hauoneshi umuhimu wala faida kwa taifa kama ambavyo kwa muda mrefu CHADEMA tumekuwa tukiuelezea kuwa unastahili kuwekwa Jumba la Makumbusho kama sehemu ya historia ya nchi yetu.

Tunauliza, kama rais aliweza kudiriki kuzuia shughuli za maadhimisho ya Uhuru na Muungano, masuala ambayo ni makubwa na yenye kubeba heshima na utu wa Mtanzania, kwa kisingizio cha kuzuia matumizi makubwa ya fedha na kuelekeza zitumike kwa shughuli zingine, tunauliza ameshindwaje kuzuia Mbio za Mwenge hadi akumbuke suala la gharama katika hatua za kuuzima? 

Kimsingi hakuna gharama ambazo Rais Dk. Magufuli amesaidia kuepuka, kwani bajeti ya posho ya siku mbili ni sehemu ndogo tu ya mabilioni ambayo tayari yameteketezwa kuzindua mbio hizo, kuukimbiza Mwenge na sherehe zenyewe za uzimaji, fedha ambazo zimeshatumika. Na kutokana na hadhi ya ugeni katika uzimaji wa Mwenge kama ambavyo yamekuwa ni mazoea sasa kupitia Serikali ya CCM, tayari kuna watumishi wa serikali wamefika Bariadi siku nyingi kuandaa shughuli hiyo.

Aidha, hiyo ni mbali na malipo ambayo Serikali imeshafanya kwa kuingia makubaliano na kandarasi mbalimbali mbalimbali zilizokuwa zimepangwa kuhudumia viongozi na shughuli yote nzima ikiwemo chakula kwa idadi na hadhi ya viongozi waliokuwa wamethibitisha kushiriki. 

Ni vema Ras Magufuli akaacha siasa nyepesi za matukio na zenye lengo la kumjengea sifa binafsi za kisiasa na kwamba atambue taasisi ya Urais aliyonayo ni kubwa na inahitaji mambo ya msingi kuliko siasa nyepesi anazozifanya kupitia matamko na makatazo yake yasiyokuwa na tija.

Imetolewa leo Alhamis, Oktoba 13, 2016 na;

Salum Mwalim
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA
Zanzibar

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx