Waziri
wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Vijana na Watu
Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ametoa siku saba kwa taasisi za serikali,
wizara, kampuni na watu binafsi kuhakikisha wanalipa madeni wanayodaiwa
na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Waziri Mhagama pia ameziagiza bodi za wadhamini za mifuko mingine ya hifadhi ya jamii, kuhakikisha zinawashinikiza wadeni wao kulipa madeni yote wanayodaiwa ili kuiwezesha mifuko hiyo kujiendesha kwa ufanisi zaidi.
Ametoa
tamko hilo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, alipotembelea miradi
ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Amemtaka
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Erick Shitindi kuhakikisha uongozi wa
mifuko unampatia ripoti ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika wote
walioshindwa kulipa madeni yao kwa mifuko yao.
“Ninafahamu
fika kuna mikataba ambayo ilisainiwa na pande zote mbili kabla ya
kutolewa kwa hiyo mikopo na makubaliano mengine hivyo naomba basi
mikataba hiyo itumike kufanikisha agizo hili,’’ alisema.
Pia
alimuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF, Profesa Samwel
Wangwe kuhakikisha anampatia ripoti muafaka ya utekelezaji wa agizo
hilo.
“Kwa
niaba ya serikali, ninataka kuona kwamba wadaiwa wote wa mifuko hii
bila kujali nafasi zao kiuchumi au kisiasa wanalipa madeni
wanayodaiwa…hii lazima ijumuishe kampuni, wawekezaji na taasisi za
serikali,’’ alisisitiza.
Awali,
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema licha ya
mfuko wake kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo majengo,
bado wateja wake wengi hawajalipa madeni wanayodaiwa na mfuko huo
ikiwemo watu binafsi, taasisi za serikali na binafsi wakiwemo pia wale
walionunua nyumba za shirika hilo.
Alisema shirika hilo, bado linadai Sh bilioni 20 kutoka kwa wapangaji wake, deni linalohusisha pia dola za Marekani milioni 1.2.
Alifafanua
kuwa kiasi kingine cha Sh bilioni 86, kinadaiwa kama adhabu kutoka kwa
waajiri walioshindwa kukamilisha makato ya wafanyakazi wao.
Madeni
mengine ni pamoja na deni la Sh milioni 42 na dola za Marekani milioni
35.9 zilizotolewa kama mikopo kwa sekta binafsi mbalimbali huku mkopo
mwingine wa Sh bilioni 38 ulitolewa kupitia Saccs na bado
hazijarejeshwa.
“Hata
hivyo, tumeanza kuchukua hatua mahsusi kulingana na matakwa ya sheria
kuhakikisha kwamba madeni yote yanalipwa,’’ alibainisha Profesa
Kahyarara.
Waziri
nchi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu, bunge ,vijana na watu wenye
ulemavu Mhe. Jenister Mhagama akiwa ameambatana na uongozi wa Shirika
la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) alipotembelea miradi ya nyumba za
NSSF iliyopo wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF Prof Samwel Wangwe. (kushoto) akizungumza
mbele ya Waziri nchi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu, bunge ,vijana
na watu wenye ulemavu Mhe. Jenister Mhagama wakati waziri huyo
alipotembelea miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni
mwishoni mwa wiki. Wengine ni pamoja na Mkurugenzi mkuu wa NSSF, Profesa
Godius Kahyarara (kulia).
Mkurugenzi
mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara (kulia) akizungumza mbele ya
Waziri nchi ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu, bunge ,vijana na watu
wenye ulemavu Mhe. Jenister Mhagama wakati waziri huyo alipotembelea
miradi ya nyumba za NSSF iliyopo wilayani Kigamboni mwishoni mwa wiki.
Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF Prof Samwel
Wangwe (kushoto).