BEKI mpya wa klabu ya Manchester City, John Stones, amekiri kuwa umahiri wa kupasia nyavu wa straika Sergio Aguero, ni tishio kwa walinzi wa timu pinzani.
Kauli ya Stones imekuja baada ya Mwargentina huyo kutupia ‘hat trick’ katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Monchengladbach.
Mabao hayo yalimfanya Aguero kufikisha jumla ya mabao tisa katika michezo miatano ya msimu huu wa 2016-17.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28, hakuwa sehemu ya kikosi cha Chama cha Wachezaji wa Kulipwa (PFA).
Lakini pia, straika huyo wa zamani wa Atletico Madrid hakunyakua Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa England.
Hata hivyo, Stones amedai kuwa kitendo cha Aguero kuishi maisha ya ‘kutojishaua’ kimemfanya kuikosa tuzo hiyo.
“Kama ataendelea kuwa kwenye ubora alionao, nina uhakika atashangaza wengi ikiwa atakosa,” alisema Stones.
Aguero amepachika jumla ya mabao 105 katika michezo 153 ya Ligi Kuu England.
Lakini pia pasi zake za mwisho zimezaa mabao 26 tangu alipotua Etihad akitokea Atletico Madrid mwaka 2011.
Nje ya soka, Aguero ni mume wa Gianinna, binti wa aliyekuwa mpachikaji mabao hatari wa timu ya Taifa ya Argentina, Diego Maradona.
Hata hivyo, Aguero na mrembo Gianinna waliachana mwaka 2012, ikiwa ni baada ya wawili hao kudumu kwa miaka minne.
Aguero ni rafiki mkubwa wa mshindi mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or, Lionel Messi, ambapo wamekuwa wakitumia chumba kimoja pindi wanapokuwa kwenye kambi ya timu ya taifa ya Argentina tangu mwaka 2005