test

Jumapili, 18 Septemba 2016

Mbakaji Watoto wa Kike Kibaha Auwawa



Kamanda wa Polisi mkoa Pwani
WANANCHI wamemuua Michael Wiliam maarufu kama Michael Dada wakimtuhumu kuwateka watoto wa kike wawili ambao ni wanafunzi kwa lengo la kuwabaka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha, mkoani Pwani na Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi jana, wananchi hao wenye hasira walimshambulia mtu huyo sehemu mbalimbali za mwili na kumsababishia kifo.

Kamanda Mushongi akielezea juu ya tukio hilo alisema kuwa lilitokea Septemba 15, mwaka huu saa 10:00 jioni katika eneo la Tumbi, Shirika la Elimu Kibaha.
Alisema mtoto wa kwanza aliyehusika katika utekaji nyara huo ana umri wa miaka 11 akiwa anasoma katika Shule ya Msingi Kibaha na wa pili ana umri wa miaka sita akiwa ni mwanafunzi wa Shule ya Chekechea ya Mama Kawili, wote wakiwa wanaishi na wazazi wao eneo la Picha ya Ndege.
"Watoto hao walikuwa wakicheza rede mtaani kwao karibu na baa ya Lekashingo kata ya Picha ya Ndege ambapo Wiliam aliwarubuni wamsindikize mtaa wa Lulanzi kwenda kuchukua mzigo wake ambao alidai aliusahau huko," alisema.
Alisema kuwa watoto hao walikubali na kuanza kuongozana naye lakini wakiwa njiani ghafla lilitokea gari aina ya Toyota Noah lenye rangi nyeusi ambalo namba zake hazikuweza kufahamika mara moja, na kusimama walipo watoto hao na baadaye walishuka watu waliojificha sura zao. Waliwabeba watoto hao na kuwaingiza katika gari huku gari hilo likiondolewa kwa kasi kuelekea upande lilipo pori la Shirika la Elimu Kibaha karibu na Shule ya Sekondari ya Tumbi.
"Baadaye wakiwa katika pori hilo ghafla mtoto mkubwa alimponyoka mtekaji nyara na kukimbia eneo lilipo bwawa la maji machafu kisha alipiga kelele za kuomba msaada ndipo kundi la watu lilipojitokeza na kuanza kumkimbiza na walipomkamata walimpiga hadi kupoteza maisha," alisema.
Alibainisha kuwa uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi umebaini kuwa Wiliam alikuwa mhalifu mzoefu na alikuwa akifanya matukio mara kwa mara ikiwemo ubakaji na wizi wa mifugo.
"Aliwahi kukamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kibaha kwa kuiba ng’ombe wanne lakini aliachiwa huru yeye na mwenzake Said Mohamed baada ya mlalamikaji kushindwa kufika mahakamani baada ya kuwapata ng’ombe wake.
Kesi iliyofunguliwa ni namba KBH/STPU/02/2014," alisema. Kutokana na tukio hilo, jeshi hilo limewataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi badala yake wawapeleke watuhumiwa kwenye vyombo vya sheria ili hatua ziweze kuchukuliwa. Pia wawe na utamaduni wa kwenda kutoa ushahidi mahakamani.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx