test

Jumatano, 14 Septemba 2016

Mishahara ya Madaktari, manesi, na walimu yafafanuliwa


SERIKALI imesema wafanyakazi wa sekta ya afya ndio wanaopokea viwango vikubwa vya mishahara wakifuatiwa na wale wa sekta ya elimu nchini.
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angela Kairuki, alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Zubeda Sakuru (Chadema).

Katika swali lake, Sakuru alitaka kujua Serikali inakabiliana vipi na changamoto za masilahi kwa watumishi katika sekta ya afya.
Sakuru alisema kuna matukio ya vifo visivyo vya lazima vinavyotokana na ukosefu wa motisha kwa madaktari na wauguzi, ambao wanalipwa viwango vidogo vya mishahara na hawalipwi posho zao kwa wakati.
Akijibu swali hilo, Kairuki alisema Serikali imeendelea na jitihada za kuboresha mishahara ya watumishi wake, ikiwamo wataalamu wa sekta ya afya kwa kuzingatia uwezo wa kifedha.
Alisema kwamba mishahara huzingatia ngazi ya elimu, ambapo ngazi ya astashahada kwa upande wa Serikali Kuu ni Sh 390,000, kada ya walimu Sh 419,000, wauguzi Sh 432,000 na madaktari ni Sh 432,000.
Kwa upande wa stashahada, Serikali Kuu ni Sh 525,000, walimu 530,000 wauguzi 680,000 na madaktari ni Sh 680,000.
Kairuki alisema ngazi ya shahada kwa upande wa Serikali Kuu ni Sh 710,000, walimu 716,000, wauguzi 980,000 na madaktari ni Sh 1,480,000.
Pamoja na hayo, alisema Serikali inaendelea na utafiti wa tathmini ya kazi na itakapokamilika, itapanga upya mishahara na motisha kwa watumishi wote wa umma ikiwamo sekta hiyo.
“Kati ya mwaka 2010/11 hadi mwaka 2016/17, vianzia vya mishahara kwa kada za wauguzi vimeongezeka kutoka shilingi 614,000 hadi 980,000 kwa mwezi kwa wahitimu wa shahada.
“Vimeongezeka pia kutoka shilingi 425,000 hadi shilingi 680,000 kwa wahitimu wa stashahada na shilingi 260,000 hadi shilingi 432,000 kwa wahitimu wa astashahada.
“Kwa kada ya madaktari na maofisa tabibu katika kipindi hicho, vimeongezeka kutoka shilingi 886,800 hadi shilingi 1,480,000 kwa wahitimu wa shahada na shilingi 425,000 hadi shilingi 680,000 kwa wahitimu wa stashahada na shilingi 260,000 hadi shilingi 432,000 kwa wahitimu wa astashahada.
“Pamoja na hayo, Serikali itaendelea kuboresha masilahi ya waatumishi kadiri uwezo wake wa kulipa utakavyoimarika,” alisema Kairuki.
Wakati huo huo, Serikali imewaagiza waajiri wote nchini kuhakikisha wanatenga fedha za uhamisho na za marekebisho ya mishahara kabla ya hatua yoyote kufanyika.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx