Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa siku mbili kwa wananchi wa mkoa wa Dar kwenda kupima afya bure na madaktari bingwa kutoka Muhimbili, Ocean Road, taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete,Agha khan na hospitali zote za rufaa mkoani Dar.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu kampeni ya kupima afya bure ambayo inaratibiwa na ofisi yake kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali za rufaa za Mkoa wa Dar es Salaam alisema:
“Leo tunataka tutumie fursa hii kuwaambia wananchi wa Dar es Salaam wamepata fursa ya kipekee ya tarehe 24 na 25 mwezi huu, siku ya Jumamosi na Jumapili katika viwanja vya Mnazi Mmoja, watakutana na madaktari wetu bingwa kutoka hospitali mbalimbali katika mkoa wetu, watakaofanya uchunguzi wa magonjwa zaidi ya kumi, ambapo kwako wewe hukatazwi kutoka eneo moja kwenda eneo jingine, unaweza ukakutana na mtaalam wa figo kutoka Muhimbili, ukatoka ukaenda kwa mtaalamu wa moyo, ukatoka ukaenda kwa mtaalamu wa saratani ya kizazi ukatoka ukaenda kwa tezi dume,”alisema.
“Bado nafasi ya kucheki afya yako kwa kiwango chote unachotaka kwa siku mbili kwa maana ya tarehe 24 na 25, tunao watu kutoka hospitali zetu za mkoa zenyewe, maana yake Mwananyamala, Ilala na Temeke, tunao wataalamu kutoka Muhimbili kutoka Muhimbili, Ocean Road, taasisi ya moyo ya Jakaya,Agha khan, kila kona wameamua kuitika japo wengine hapa hawaonekani lakini watakuwepo ili kuhakikisha wanakupa huduma ili wewe uweze kufanikiwa. Ni fursa ya kipekee sana ambayo madaktari wetu wametupa kwa moyo wa upendo kabisa kwasababu gharama ni kubwa,” alisisitiza.
“Sio tu gharama pia wanaacha kazi zao zingine, wanaacha kukaa na familia zao kwa siku za wikiendi wanakuja kujitolea kwako wewe mwananchi wa mkoa wa Dar es Salaam. Kwahiyo naomba nitoe wito kwa wakazi wote wa Dar es Salaam katika malango yote, katika pembe zote za mkoa wetu, kazi yako sasa ikibaki ni kuchukua nauli yako kuingia kwenye daladala, kuchukua gari lako kuingia kwenye usafiri wako na kuhakikisha unafika mnazi mmoja sa mbili asubuhi kwaajili ya kupata huduma hii,” alisema Makonda.