KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewasilisha tuhuma sita dhidi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye amefukuzwa uanachama.
Maalim Seif aliwasilisha hoja hizo mbele ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho kilichofanyika jana mjini Unguja visiwani Zanzibar, ambapo wajumbe walitumia Katiba ya CUF, Ibara 10(1)(C), kumfukuza uanachama Profesa Lipumba.
Wakati Baraza Kuu likichukua hatua hiyo, Profesa Lipumba alitumia siku ya jana kuendesha kongamano lililofanyika Buguruni jijini Dar es Salaam, ambapo amepinga uamuzi huo na kusema kuwa kikao hicho ni batili kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi, Mwenyekiti wa kikao hicho, Katani Ahmed , alisema walijadili kwa kina mashtaka dhidi ya Profesa Lipumba kutokana na kile alichodai hujuma alizofanya Ofisi Kuu za CUF Buguruni jijini Dar es Salaam Septemba 24, mwaka huu.
Alisema kutokana na hali hiyo Baraza Kuu limepokea mashtaka dhidi ya Prof. Lipumba yaliyoandaliwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ambayo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, Ibara ya 108 (1) ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia nidhamu ya chama katika ngazi ya Taifa na kuyawasilisha mapendekezo yake mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
“Baraza Kuu limeridhika kwamba Kamati ya Utendaji ya Taifa imefuata masharti yote ya katiba ya chama ya 1992 (Toleo la 2014) katika kuandaa mashtaka hayo kutokana na mtuhumiwa, Prof. Ibrahim Lipumba, kuvunja katiba ya chama, Ibara ya 12 inayohusu ‘Wajibu wa Mwanachama” hasa Ibara ndogo za 12 (6), 12(7) na 12(16).
“Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeridhika kwamba Kamati ya Utendaji ya Taifa ilimfikishia mtuhumiwa, Prof. Ibrahim Lipumba, barua ya wito Kumb. Nam. CUFHQ /OKM /WM /2016 /Vol.1 /49 ya Septemba 24 mwaka huu ambayo pia ilikuwa na maelezo ya tuhuma na kumtaka afike mbele ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kilichofanyika leo (jana) kuja kujieleza na kujitetea kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa katiba ya chama kwa kuvunja masharti yanayohusu “Wajibu wa Mwanachama”,” alisema Katani .
Mwenyekiti huyo wa kikao ambaye pia ni Mbunge wa Tandahimba, alisema Baraza Kuu limesikitishwa na dharau iliyooneshwa na Prof. Lipumba dhidi ya kikao hicho ambacho ni chombo cha juu chenye mamlaka ya kusimamia uongozi wa chama licha ya kupelekewa wito wa kumtaka afike mbele yake.
Alisema kitendo cha dharau kinaonesha jinsi gani heshima na uaminifu wa Prof. Lipumba kwa chama ulivyoshuka na wameridhika kwamba kwa kuwa Prof. Lipumba akiwa mtuhumiwa alichagua mwenyewe kudharau wito wa kufika kujieleza na kujitetea ambayo ni haki yake kama mwanachama kwa mujibu wa Ibara ya 11(6) ya katiba ya chama, halikuwa na sababu ya kutoendelea kumjadili na kuchukua hatua dhidi yake.
“Baraza Kuu limeridhika na mashtaka dhidi ya Prof. Ibrahim Lipumba kwamba kwa kitendo chake cha kuongoza na kusimamia kikundi cha wahuni kuvamia Ofisi Kuu ya chama, Buguruni, Dar es Salaam, siku ya Jumamosi, Septemba 24 Septemba, 2016 na watu hao aliowaongoza na kuwasimamia kupiga walinzi waliokuwepo.
“Kuvunja na kuharibu mali za chama na hivyo kuharibu heshima na taswira ya chama mbele ya jamii ndani na nje kwamba ametenda makosa kinyume na “Wajibu wa Mwanachama” kama ilivyoelezwa kwenye Ibara ya 12(6), 12(7) na 12(16) za katiba ya chama.
“Baada ya kuridhika na mashtaka hayo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeamua kwa kutumia uwezo wake kwa mujibu wa Ibara ya 10 (1) (c) na kwa kura zote 43 za wajumbe wake waliohudhuria kumfukuza uanachama Prof. Ibrahim Lipumba, kuanzia leo (jana).
“Kwa maamuzi haya, Baraza Kuu linaweka bayana kwa wanachama wa CUF, Watanzania na mamlaka zote nchini kwamba kuanzia leo, Prof. Ibrahim Lipumba hana haki ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na shughuli zozote za chama,” alisema Katani.
Pamoja na hali hiyo alisema CUF inawapa pole wanachama wake walioathirika kutokana hatua ya msajili kuingilia mambo ya chama kinyume na uwezo alionao na pia kwa matendo ya kihuni yaliyofanywa na Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake kuvamia ofisi kuu ya chama hicho.