Bi Clinton alizidiwa na nusura azirai alipokuwa anahudhuria hafla ya kuadhimisha miaka 15 tangu kutekelezwa kwa shambulio la kigaidi la 9/11 ambapo watu karibu 3,000 waliuawa.
Aligunduliwa kuwa anaugua kichomi, ugonjwa wa mapafu ambao pia hujulikana kama nimonia, siku ya Ijumaa.
Kumezuka mjadala mkali kuhusu afya yake Marekani, na muda ambao alichukua kupata nafuu, huku uchaguzi mkuu ukiendelea kukaribia.
Amekuwa akikosolewa kwa kushindwa kutoa taarifa zake mapema mpaka pale alipokaribia kuanguka mbele ya hadhara katika siku ya kumbukumbu ya shambulizi la Septemba 11.
Akihojiwa na shirika la habari la CNN, Bi Clinton amesema kuwa hakufuata vyema kile anachokiita ushauri wa madaktari wake wa kupumzika kwa siku tano baada ya kufanyiwa vipimo siku ya Ijumaa.
Timu yake ya kampeni imesema kuwa hana tatizo lolote la kiafya isipokuwa homa ya mapafu na kuongeza kuwa taarifa zaidi juu ya uimara wa afya yake zitatolewa.