Mfanyabiashara
Ndama Shabani Hussein maarufu kama ‘Pedezyee Ndama Mtoto wa Ng'ombe’,
jana alikiri kwa mara ya tatu shtaka la kutakatisha fedha dola za
Marekani 540,000 baada ya upande wa utetezi kuomba mshtakiwa kukumbushwa
mashtaka yake.
Awali,
Mei 23 mwaka huu, Ndama alikiri kosa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
ilipanga kusikiliza maelezo ya awali Mei 29, lakini aliomba muda wa
kujadiliana na mawakili wa utetezi hadi Mei, 30, mwaka huu
alipokumbushwa mashtaka yake na kukana kutakatisha fedha hizo.
Hata
hivyo, hali ilikuwa tofauti jana katika mahakama hiyo iliyoketi jana
chini ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, baada ya Ndama kuomba
kukumbushwa mashtaka yake na aliposomewa, alikiri kwa mara nyingine
kutakatisha fedha hizo.
Wakili
wa Serikali, Esterzia Wilson, alimkumbusha Ndama mashitaka
yanayomkabili baada ya wakili wa utetezi, Jeremiah Ntobesya, kuomba
mteja wake kukumbushwa mashitaka hayo.
Mahakama
iliridhia ombi hilo na aliposomewa hati ya mashtaka sita, alikana
mashtaka matano na kukiri shtaka la sita la kutakatisha fedha.
Katika
shitaka la kutakatisha fedha, Ndama anadaiwa kuwa kwa tarehe tofauti
jijini Dar es Salaam, kati ya Februari 26 na Machi 31, 2014, akiwa
mwenyekiti na mtiaji saini pekee wa kampuni ya Muru Platnum Tanzania
Investment Company Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko
benki ya Stanbic, alijihusisha moja kwa moja katika uhamishaji fedha
dola za Marekani 540,000.
Ilidaiwa
kuwa alizitoa fedha hizo taslim huku akijua au alipaswa kujua kuwa
fedha hizo ni za kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Hata
hivyo, Ndama alikana mashitaka mengine ikiwamo la kudaiwa kuwa Februari
20,2014, akiwa jijini Dar es Salaam, alighushi nyaraka ya kibali cha
kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonyesha kuwa
kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa
kusafirisha maboksi manne ya dhahabu ya kilogramu 207, yenye thamani ya
Dola za Marekani 8,280,000 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL
DTYL Limited wakati akijua si kweli.
Pia
Ndama anadaiwa kuwa Machi 6, 2014, Dar es Salaam, alighushi kwa
kutengeneza hati ya kibali cha Umoja wa Mataifa Ofisi ya Dar es Salaam,
akijaribu kuonyesha kuwa kilogramu 207 za dhahabu kutoka nchini Congo
zinazotarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania
Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL
PTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai
yoyote wakati akijua ni kosa kisheria.
Aidha,
anadaiwa kuwa Februari 20, 2014, alighushi fomu ya forodha yenye namba
za usajili R.28092 akionyesha kampuni ya Muru imeilipa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa
bidhaa ambazo zina uzito wa kilogramu 207 za dhahabu zenye thamani ya
dola za Marekani 8,280,000 kutoka Congo.
Katika
shitaka jingine, Ndama anadaiwa kuwa Februari 20, 2014, alighushi
nyaraka ya bima kutoka Phoenix of Tanzania Assurance Company Ltd,
akionyesha kampuni ya Muru imeyawekea bima makasha manne yaliyokuwa na
dhahabu hizo.
Anadaiwa
kuwa kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014, akiwa Dar es Salaam, kwa
njia ya udanganyifu alijipatia kutoka kwa kampuni ya nchini Australia ya
Trade TJL DTYL Limited dola za Marekani 540,000 baada ya kudanganya
atawapa na kusafirisha dhahabu hizo.
Awali, Ndama aliposomewa maelezo ya awali, baada ya kukiri kosa hilo, alikana maelezo mengi ya msingi yanayounda shitaka hilo.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Nongwa aliamuru kesi hiyo kuendelea kusikilizwa kwa kuwa nia ya Ndama ya kukiri kosa
ilikuwa na shaka.
0 comments:
Chapisha Maoni