Ikiwa
zimepita siku kadhaa tangu Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi
(CUF) kutuhumu baadhi ya viongozi wake waliosimamishwa uanachama kupanga
njama za utekaji viongozi wa chama hicho, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam linawashikiliwa wanachama wa CUF 22 kwa tuhuma za
kupanga njama za kufanya fujo na kuchoma mali za ofisi za chama hicho.
Ikumbukwe
kuwa, Septemba 16,2016 CUF kupitia Kurugenzi yake ya Habari na Uenezi
ilitoa taarifa ya jaribio la utekaji wa Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha
CUF, Joran Bashange ambapo chama hicho kiliwatuhumu Magdalena Sakaya,
Abdul Kambaya na Profesa Ibrahim Lipumba kuwa walinzi wao walijaribu
kufanya tukio hilo.
Kamishna
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro jana
alisema wanachama hao walikamatwa na zana za kufanyia uhalifu yakiwemo
mapanga, Jambia, visu na chupa za kupulizia 10 zikiwa kwenye boksi lenye
maandishi ya lugha ya kichina.
Watuhumiwa
hao walikamatwa Septemba 25,2016 maeneo ya Mwananyamala katika gari ya
abiria ambayo ruti yake inapitia njia ya Buguruni-Mwananyamala.
Kamanda
Sirro alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya askari kupata taarifa
kwamba wamekuja Dar es Salaam wakitokea visiwani Unguja kutoka katika
matawi mbalimbali ya chama hicho kwa lengo la kufanya fujo.
Aidha,
Sirro alisema baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa, walieleza kuwa wamekuja
kutokana na maelekezo ya kiongozi wa CUF Nassoro Ahmad Mazrui ambaye ni
Naibu Katibu mkuu wa chama hicho aliyewataka kuungana na walinzi wenzao
waliopo katika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni.
Hata
hivyo, baada ya taarifa za watuhumiwa hao kukamatwa kuenea katika
mitandao ya kijamii, baadhi ya watu walimhusisha aliyekuwa mwenyekiti wa
kamati ya uongozi wa CUF kwa muda Julias Mtatiro kuhusika katika
mipango ya njama hizo.
Lakini Kamanda Sirro alieleza kuwa hadi sasa hajapokea taarifa hiyo ya kuhusika kwa Mtatiro na kwamba taarifa hizo si za kweli.