Polisi
wamewatia mbaroni watu watano wanaodaiwa kusambaza taarifa kwenye
mitandao ya jamii kuwa Mbunge wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon
Ndesamburo amefariki dunia.
Miongoni
mwa waliokamatwa na kuhojiwa na polisi na simu zao kushikiliwa kwa
uchunguzi, ni wanachama wa Chadema na maofisa wa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).
Kamanda
wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa jana alisema kuwa,
uzushi huo kuwa Ndesamburo amefariki dunia, ulisambazwa zaidi kupitia
makundi ya WhatsApp.
“Tarehe
29/7/2016 mzee Ndesamburo alifika polisi na kutoa taarifa kuwa katika
mitandao ya jamii kuna taarifa na picha yake, inasambazwa kwa kasi kuwa
amefariki dunia,” alisema Mutafungwa na kuongeza:
“Picha
hiyo ilikuwa na maneno RIP (Rest in Peace), wakimaanisha apumzike kwa
amani. Tulifungua jalada na kitengo chetu cha Cyber Crime (makosa ya
kimtandao) kiliingia kazini.”
Alisema watu mbalimbali walihojiwa na polisi wanaendelea kazi hiyo pia watu watano walikiri kupokea ujumbe huo na kuusambaza.
Kamanda
Mutafungwa alisema wanaendelea na uchunguzi wa kisayansi kumpata mtu
aliyeanzisha ujumbe huo, ambao ulisababisha usumbufu kwa Ndesamburo na
familia yake.
Wanaoendelea
kuhojiwa ni Ofisa Usalama wa Kampuni ya Kilimanjaro Airport Development
(Kadco) na msimamizi wa waongoza ndege wa Fast Jet Uwanja wa Kia.
Wengine
ni wanachama watatu wa Chadema, ambacho Ndesamburo ni Mwenyekiti wake
wa Mkoa Kilimanjaro. Katibu wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema
alithibitisha kuhojiwa kwa wanachama wake na kwamba, anaamini
mwanzilishi wa taarifa hiyo ya uzushi hajakamatwa.