test

Jumatatu, 29 Agosti 2016

Serikali yapiga marufuku uuzaji wa ardhi zinazomilikiwa kimila


Serikali imepiga marufuku uuzaji wa ardhi zinazomilikiwa kimila kupitia mikataba ya muda mrefu kwa watu binafsi au taasisi, kwa kuwa sehemu kubwa ya ardhi inayomilikiwa na vijiji kwa sasa ndio imegeuzwa shabaha kubwa ya wawekezaji wa nje na wa ndani.
Maneno hayo yalisemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wakati akihojiwa katika kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ kinachorushwa na TBC 1. Alisema kuwa kuanzia sasa hakuna kijiji chochote kitakachoruhusiwa kuwasilisha maombi ya kubadili umiliki au kuuza ardhi kwa sababu yeyote ile hata kama ni kwa matumizi ya umma.
“Ni marufuku wageni au wawekezaji kwenda vijijini moja kwa moja kununua ardhi, waje kwangu au wapitie Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) tutawapa ardhi haraka wawekeze,” alisisitiza.
Aidha Lukuvi ambaye alionesha kusikitishwa na tatizo lililokithiri na la muda mrefu la migogoro ya ardhi nchini, alisisitiza kuwa uamuzi wa kusitisha kuuzwa kwa ardhi hizo, pia ni njia mojawapo ya kupunguza migogoro hiyo.
Waziri wa ardhi aliweza kueleza haya pia kwa upande wa wizara yake, “wizara yangu pia imetenga viwanja 240 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika mji wa Kigamboni na nasisitiza anayetaka viwanja kwa ajili ya kuendeleza viwanda awasiliane nami na atavipata viwanja hivyo bila rushwa wala ubabaishaji.
“Nasisitiza mtu anayetaka kujenga kiwanda popote pale aje kwangu nitampatia ardhi ndani ya siku saba, pamoja na hayo, nasema hivi kuna baadhi ya watu wamekuwa hawaniungi mkono kwa kuwa niliwanyang’anya ardhi zao. Hili halitonizuia nitaendelea kuzichukua ardhi zote ambazo haziendelezwi na wawekezaji bila kujali wao ni akinanani wala uraia wao,” aliongezea.
Kuhusu ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni, alisema bado mchakato wake unaendelea na wizara hiyo imekuwa ikipokea mawazo ya wadau mbalimbali kuhusu ujenzi wa mradi huo ambayo inayapokea na kuyafanyia kazi.
CHANZO: HABARI LEO

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx