test

Alhamisi, 4 Agosti 2016

RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 26


MTUNZI: ENEA FAIDY

....BI CAROLINA alipiga hatua za taratibu kuelekea sebuleni lakini hali iliyokuwemo ndani mle ilizidi kumshangaza kwani alisikia harufu Kali na mbaya ya kitu kuungulia. Alifika sebuleni lakini hakukuta Mtu yeyote, akaamua kwenda jikoni....
 
Alipoingia jikoni tu, alipiga chafya tatu mfululizo kutokana na moshi mzito ulioambatana na harufu Kali sana uliotawala jikoni mle. Aliisogelea mpaka sehemu ya kupikia akagundua moto uliwashwa na kuna kitu kilichomwa. Akaangalia sufuria zote lakini hakukuta kitu chochote, akabaki na mshangao.
"Doreen!" Aliita Bi Carolina akiwa ameshika mkono kiunoni.
"Abee mama!" Sauti ya Doreen ilisikika kutoka chumbani.
"Njoo huku jikoni"
 
Bila ya kuchelewa Doreen alifika jikoni kule na kumkuta Bi Carolina akiwa ameshika kiuno akimsubiri kwa hamu amuulize kilichotokea.
"Abee mama" aliitikia Doreen kwa adabu sana.
"Nini kimetokea huku jikoni?"
"Nisamehe mama... Nilitaka kupika.. Ila kwa bahati mbaya nikaunguza kwani sijui kutumia jiko la gesi." Alijitetea Doreen huku akitia huruma sana.
 
"Ulitaka upike nini asubuhi yote hii?"
"Nili...nilikuta maziwa.. Nyama kwenye friji nikataka nipike.."
"Mara maziwa mara nyama.. Mbona sikuelewi? Haya ulipikia sufuria gani?" Bi Carolina alishindwa kumuelewa Doreen ila kutokana na ugeni aliokuwa nao hakuweza kumfokea sana kwa kuhofu kuwa atajisikia vibaya.
"Nilichukua nyama... Sufuria ilipoungua sana nikaamua kuiosha.." Alisema Doreen akidai kutetemeka kwa woga.
"Sawa ila usirudie tena.. Nitakufundisha jinsi ya kupikia jiko la gesi.."
"Sawa mama" alisema Doreen kwa sauti ya upole iliyojaa hekima ya viwango vya juu.
"Sawa mwanangu nenda kaendelee na kazi zako"

Doreen alitoka jikoni mle na kuelekea chumbani kwake. Alichukua kimfuko cheusi kidogodogo kisha akafungua na kuutoa ungaunga mweusi. Kisha akaweka kiganjani na kusogelea kila kona ya chumba kile na kuupuliza kwa midomo yake. Alifanya hivyo mpaka unga ule ilipoisha, akasogelea kitanda chake na kukaa.
 
"Hapa sasa nimemaliza kazi... Mpaka huo moshi uishe nitakuwa nimefanikiwa kabisa." Alisema Doreen akitabasamu kwani ule moshi uliotapakaa ndani mle ulisababishwa na Doreen. Alikuwa amechoma dawa ambayo ingewafanya wakaaji wa nyumba ile kumpenda Doreen kupita kiasi, na wasingeweza kumfukuza hata iweje mpaka pale atakapoamua kuondoka yeye mwenyewe.

Aliangalia SAA yake ya mkononi ilikuwa tayari ni saa nne na nusu asubuhi. Doreen alisikia sauti ya Bi Carolina ikimwita. Akatii wito na kumfuata Bi Carolina.
"Abee mama" aliitikia kwa heshima.
"Umeoga?"
"Bado"
"Kaoge unywe chai."
"Sawa mama"
Doreen alitoka sebuleni pale na kwenda bafuni kuoga. Alipomaliza alipaka mafuta na kuvaa tena nguo alizokuwa amevaa kabla ya kuoga kisha akaenda sebuleni. Akamkuta Bi Carolina akiwa amekaa huku akitazama televisheni.
"Mbona umevaa nguo chafu?"
"Sina zingine"
 
"OK.. Baadae tutaenda Mwanjelwa ukatafute nguo za kuvaa.. Sasa hivi nenda ukanywe chai.." Alisema Bi Carolina.
"Sawa mama.. Vipi kuhusu Dada Pamela?" Aliuliza Doreen.
"Atakuja si muda mrefu.. Ameniambia yupo njiani. Baada ya kumwambia hivyo ghafla mlango ukagongwa . Akaingia msichana mmoja mrefu kiasi, mweupe, matiti yenye ukubwa kiasi, kiuno chembamba kama sindano na makalio makubwa kama milima miwili iliyopangana vyema. Wote walishtuka kidogo.
"Ah Pamela kumbr ulikuwa jirani tu.. Tumekuongelea sasa hivi hapa.."
 
"Sikuwa mbali"
"Karibu sana" alisema Bi Carolina wakati huo Pamela alikuwa akiketi sofani na kuweka pembeni mkoba wake. Kwa muda wote huo Doreen alikuwa akimtazama Pamela katika maeneo ya kifuani.
"Shkamoo Dada Pamela" alisalimia Doreen
"Marhaba hujambo? Wewe ndo Doreen?"
"Ndio.." Aliitikia Doreen huku akimgeukia mama Pamela "kumbe una mtoto mzuri namna hii?" Alisema.
Bi Carolina na Pamela walicheka tu.
"Huyu ndo mwanangu mpenzi... Yuko peke yake kama Tanzanite..." Alisema Mama Pamela huku akicheka.
Doreen aliwaacha wakiendelea na mazungumzo kisha yeye akaenda chumba cha kulia chakula (dinning). Moyoni mwake alifurahi sana kwani kwa uzuri aliokuwa nao Pamela titi lake lilifaa sana kwa kazi ya Doreen.

********
Dorice aliitazama Pete ya Mansoor kwa mshangao kwani hakujua lengo kamili la Mansoor kutaka kuitazama Pete ile.
"Umeitazama vizuri Pete hiyo?"
"Ndio"
"Hii Pete, si kama Pete za kawaida, ina nguvu nyingi sana ambayo inazidi nguvu za kaeaida." Alisema Mansoor kisha akakohoa kidogo ili kusafisha koo lake kisha akaendelea.
 
"Pete hii nilipewa na babu yangu ambaye anaishi mbali sana katika sayari nyingine kabisa, alinipa kwaajili ya ulinzi wangu binafsi kwasababu alikuwa ananipenda. Na Mimi nitakupa wewe pete hii kwasababu nakupenda sana, ili ikusaidie katika kumuokoa mtu umpendae sana." Alisema Mansoor huku akimtazama Dorice. Dorice aliendelelea kumsikiliza kwa umakini sana Mansoor.
"Pete hii ni ya ufalme wangu pale nitakapopewa ufalme na mama yangu... Wewe kwasababu ni mke wangu utakuwa malkia..."
"Nini?"
 
"Unashangaa nini? Sina njia nyingine ya kukusaidia mbali na hii.. Kama upon tayari nitakupa pete hii na utakuwa na uwezo mkubwa sana wa kijini... Utarudi duniani na utafanya kila unalotaka..." Alisema Mansoor. Maneno yake yalikuwa mazuri masikoni mwa Dorice ingawa yalimpa utata wa kiwango cha juu alijiuliza maswali mengi kichwani mwake juu ya suala la umalkia. Lakini akayapotezea maswali yake kwani alitamani sana kurudi duniani kumuokoa mpenzi wake Eddy na kwenda kwa wazazi wake ambao hakuwaona kwa muda mrefu.
"Sawa... Nipe tu..!" Alisema Dorice akionesha kukubali masharti ya Mansoor.
 
"Nitakupa Mke wangu lakini kuna jambo muhimu unalotakiwa kuzingatia pindi utakapokuwa na hii pete"
"Jambo Gani?" Dorice alishtuka.
"Hii ni pete ys heshma sana, ambayo haihitaju uchafu wa aina yoyote.. Kwahiyo ukiivaa na kwenda Nayo duniani hutakiwi kufanya mapenzi na mwanaume mwingine zaidi yangu Mimi!" Alisema Mansoor huku akimtazama mkewe kwa macho yaliyoonesha msisitizo kwa kile alichokizungumza.
 
"Mmh!" Aliguna Dorice kwani alikuwa na wazo la kumsaliti Mansoor pindi atakaporudi duniani. Na alikuwa na lengo la kutorudi tena katika himaya ile ya majini. Hivyo basi masharti ya pete ile yalikuwa magumu sana kwake na kumuweka katika wakati mgumu sana.
"Mbona unaguna?"
"Kwani hakuna msaada mwingine mbali na hiyo pete" aliuliza Doreen
"Upo!"
"UPI.. Nipe msaada mwingine Mansoor tafadhali"
"Unataka njia nyingine?"
"Ndio.." Alijibu Dorice haraka.

**********
Mr Aloyce alitembeatembea katika eneo lile akimsubiri mkewe atokeze lakini muda ukazidi kwenda Vila kuona dalili yoyote. Mr Aloyce alianza kukata tamaa ya kumpata mkewe akahisi huenda alikuwa anadanganywa tu. Akataka kuondoka lakini moyo wake ulisita sana baada ya kuumbuka msemo usemao "atafutaye hachoki, akichoka keshapata" akaamua kuwa mvumilivu kwani siku zote mvumilivu hula mbivu.
 
Ajasogelea eneo tulivu lenye nyasi fupi kisha akaketi pale. Mawazo mengi yalifurika kichwani mwake, "nimekuwa mtumwa... Mtumwa wa nguvu za giza hii hali mpaka lini? Kila siku yanaibuka mapya... Mmh! Yote hii ni kwasababu ya Eddy.. Ila sipaswi kumlaumu" alijiwazia Mr Alloyce huku machozi yakimtiririka.
 
Ghafla upepo mkali ulianza kupuliza eneo lile na kumwondoa mawazoni Mr Aloyce. Alinyanyuka pale chini na kutazama juu lakini hakuona chochote.
 
Upepo ukazidi kupuliza kwa kasi sana mpaka miti ikaanza kuyumbayumba. Miti iliyumba kwa kasi sana na ile isiyo na nguvu ikaanguka. Mr Aloyce aliogopa sana.
Baada ya upepo ule radi Kali zikapiga mfululizo, zikazidi kumtisha Mr Aloyce. Alipiga hatua kuelekea kwenye gari yake ili akajifiche mle maana hali ilitishs lakini ghafla akasikia sauti ya kilio kikali.
 
"Nisaidie mume wangu.. Nisaidiee!" Mr Aloyce alishtuka sana kwani sauti ile aliijua fika. Ilikuwa ni sauti ya mkewe mpenzi. Akabaki amesimama wima kama mlingoti ili asubiri kitakachoendelea.
Akiwa bado amesimama alishtushwa na kitu kikipita miguuni mwake, akatulia kimya huku akipiga jicho kutazama kilikuwa kitu gani.
 
"Mamaaa" mr Aloyce alipiga ukunga kwa woga na hofu baada ya kuonana uso kwa uso na chatu aliyekuwa akijiviringa kwa kasi mwilini mwake.
Itaendelea.....

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx