MWANAMKE
anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40, amekutwa amekufa katika
mazingira yanayoonesha kwamba alibakwa kabla ya kuuawa na kutupwa
kichakani.
Mwili
wake ulionekana Agosti 10, mwaka huu saa 7.30 mchana katika Kijiji cha
Iringa Mvumi, Kata ya Mvumi, Wilaya ya Chamwino Mkoa wa Dodoma.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa amesema kwamba wanamfanya
msako waliotenda unyama huo ili wawafikishe katika mkondo wa sheria.
Alitoa
mwito kwa wakazi wa Kijiji cha Iringa Mvumi na vijiji vya jirani
kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua wahalifu hao ili wachukuliwe
hatua za kisheria.
Wakati
huo huo, Mahakama ya Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma imemtupa jela
miaka 30 mkazi wa Kijiji cha Mlali Iyengu, Mkengela Mchechele (27) baada
ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 11.
Akitoa
hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kongwa,
Mary Senapee pamoja na kumtupa jela miaka hiyo, pia aliamuru mtuhumiwa
kuchapwa viboko 12 na akitoka jela alipe fidia ya Sh milioni moja.