Waziri
wa Mambo ya Katiba na Sheria Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe amesema amri
ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya nje na ndani ya vyama vya
siasa ni halali ambayo kila Mtanzania na mwanachama wa chama chochote
cha siasa anapaswa kuitii na kuizingatia na kwamba kutokufanya hivyo ni
kuvunja sheria za nchi.
Amesema
amri hiyo ni ya kudumu ambayo imelenga kuangalia na kufanya tathmini ya
hali ya nchi kutokana na viashiria mbalimbali vya uvunjifu wa amani
nchini ambavyo vimeanza kuonekana.
Dkt
Mwakyembe alikuwa akijibu swali kutoka kwa Kituo cha Televisheni cha
Taifa TBC 1 ambacho kilitaka kupata ufafanuzi kuhusiana na uhalali wa
kauli ya Jeshi la Polisi ya kuzuia mikutano ya ndani na ya hadhara kwa
vyama vya siasa nchini.
“Jeshi
la Polisi ni chombo halali cha cha dola kilichoanzishwa kisheria chenye
wajibu wa kulinda usalama wa raia na mali zake ndani ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, na kuongeza kuwa uamuzi huo una lengo la kulinda
amani ya nchi na endapo kutakuwa na viashiria vya kutishia amani ya nchi
yetu lazima hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe. Ni amri halali
na kila Mtanzania na mwanachama wa chama chochote nchini anapaswa kuitii
na kuizingatia na kwamba kwenda kinyume ni kukiuka sheria, ” alisisitiza Mhe. Mwakyembe.
Mhe.
Waziri amesema ni haki ya vyama vya siasa kufanya mikutano ila
wanatakiwa kutoa taarifa Polisi ili waweze kutoa ulinzi wakati wa
mkutano huo na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi linaweza kuzuia mikutano
hiyo kwa sababu za kiusalama.
Mhe.
Waziri pia alisema sio kweli kuwa Mhe. Rais amezuia mikutano ya siasa,
bali alichofanya ni kudhibiti uendeshaji wa holela au huria wa shughuli
za siasa nje ya maeneo ya uchaguzi ya wanasiasa na kuongeza kuwa Mhe.
Rais amefanya hivyo kutokana na kiapo chake cha kuilinda, kuihifadhi na
kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taifa kwa ujumla.
“Mhe.
Rais hajapiga marufuku siasa, alichofanya ni kudhibiti uendeshaji
holela au huria wa shughuli za siasa nje ya maeneo ya uchaguzi ya
wanasiasa husika kuepusha shari na chuki na amefanya hivyo kutokana na
kiapo chake cha kuilinda, kuihifadhi na kuitetea Katiba ya Tanzania na
taifa kwa ujumla wake. Kwa hatua hiyo Mhe. Rais hajafunga milango ya
majadiliano. Milango iko wazi na tulitegemea wenzetu wangekuja na njia
mbadala na kulizungumzia hilo badala ya kuitisha maandamano ya nchi
nzima," alisema.
Mhe
Mhe. Waziri amevitaka vyama vya upinzani nchini kukaa na kuzungumza na
Serikali na kuacha kufanya vitendo vya kutishia uvunjifu wa amani kama
kuitisha maandamano kwa nchi nzima.
“Njooni
tukae tuzungumze tupime ushauri wenu, hili ni taifa letu sote na
milango iko wazi, tuache kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani kama
ambavyo inavyoonekana nchini hivi sasa,” alisisitiza.
Amasema
Sheria ya Vyama vya siasa hairuhusu kufanyika kwa maandamano kwa nchi
nzima, kufanya hivyo ni kuchochea wananchi kuasi “civil disobedience” ni
kinyume cha sheria na serikali haiwezi kuivumilia hali hiyo.
Mhe.
Waziri ametoa wito kwa Watanzania wote kutoshiriki maandamano ya Ukuta
ambayo alisema hayatakuwa na tija kwa nchi bali kuleta vurugu katika
jamii.