CHAMA
cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kimesema kitasitisha huduma ya
kusafirisha abiria kwenda mikoa yote nchini Jumapili ili kufanya ukaguzi
wa mabasi yake, hatua ambayo itakuwa sawa na mgomo.
Aidha,
Taboa imesema inapinga uamuzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa
Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kutangaza kuyafungia mabasi yote ya
kampuni ya City Boy badala ya moja ambalo lilisababisha ajali mkoani
Singida hivi karibuni.
Julai
4, mabasi mawili ya kampuni hiyo yaligongana uso kwa uso na kusababisha
vifo vya watu zaidi ya 30 wilayani Manyoni mkoani Singida.
Taboa
imesema pia itaipeleka serikali mahakamani kutokana na kufungiwa kwa
mabasi hayo kwani kwa mujibu wa sheria, aliyetakiwa kulifungia ni waziri
mwenye dhamana na si Sumatra kama ilivyofanyika.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kumaliza
kikao cha dharura cha wamiliki wa mabasi ya mikoani, Katibu wa Taboa,
Enea Mrutu, alisema hawatakatisha tiketi kuanzia Jumapili ili kujipa
muda wa kukagua mabasi yao kama yana uwezo wa kufanya safari ama la.
"Tumeamua
kwa pamoja kuwa, kwa sababu tayari tumeshafanya 'booking' ya abiria,
kuanzia Agosti 21 mwaka huu, tuanze kufanya ukaguzi wa mabasi yetu kote
nchini ili yale ambayo hayana sifa yakae pembeni na yale yanayostahili
kusafirisha abiria yafanye hivyo, kuliko utaratibu huu wa serikali wa
kuyafungia yote bila kujali gari lililohusika kwenye ajali," alisema Mrutu.
Aidha
alisema wanapinga vikali agizo la Sumatra la kuyafungia mabasi 60 ya
kampuni 12 kwa makosa ya kusababisha ajali na wanataka mabasi
yanayohusika pekee ndio yafungiwe.
Alizitaja
kampuni zilizofungiwa mabasi yake kuwa ni Mohamed Trans, City Boy, Ota
High Class, Kisbo Safari, Kisbo Express, Lubonelo na Kanda Safari.
Mrutu
pia alisema kikao kicho kilipinga azimio la serikali kutaka mabasi
yanayoenda masafa marefu kama mikoa ya Mwanza na Mbeya kutumia siku
mbili na badala yake yatumie siku moja kama ilivyokuwa awali.
Alitaja
azimio la tatu kuwa ni kufunga mfumo maalum wa udhibiti wa magari (Car
Track System) ambao utaunganishwa na ule wa Sumatra ili kuliona gari
lilipo kwa lengo la kudhibiti ajali.
Aidha,
Mrutu alisema wamekubaliana mabasi yote yatatembea kilometa 80 kwa saa
moja na 50 pale inapohitajika kama kwenye matuta ili kuepuka ajali.
Alisema
wamekubaliana pia dereva atakayehusika kutembea zaidi ya mwendo
waliokubaliana, afukuzwe kazi na kumchukulia hatua stahiki.
"Kama
magari yetu tutayafanyia ukaguzi na pia kufunga kifaa cha kulionyesha
basi na kupunguza mwendo, hakuna haja tena ya kutaka tusafiri zaidi ya
siku moja... maeneo wanayoona kuna hatari ya usalama ni bora
yakasubiriana na askari wakayasindikiza mpaka yanapokwenda," alisema.
Aliendelea
kueleza kuwa wamekubaliana Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama
Barabarani, Mohamed Mpinga, awahakikishie hakuna askari atakayedai
mabasi hayo rushwa.
Mrutu
alisema wamekubaliana mabasi yasikaguliwe kila kituo ili kuepuka
kupoteza muda wakati wakisafiri kwenda mikoani ambako kunasababisha
madereva kutembea mwendo kasi ili kuokoa muda waliopoteza njiani.