Rais John Magufuli anatarajia kufanya ziara wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambako atafanya mkutano wa hadhara kuwashukuru wananchi kwa kumpigia kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliopita.
Mkuu
wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkulu alisema jana kwamba Rais Magufuli
atawasili hapa Jumamosi jioni kabla ya kufanya mkutano wa hadhara
Jumapili.
Nkulu
aliwataka wananchi wa Kahama na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi
kumlaki kiongozi huyo katika ziara hiyo ambayo alisema: “Lengo lake ni kuwapongeza wananchi wa Kahama kwa kumpa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika mwaka jana.”
Alisema ziara hiyo ni muhimu kwa kuwa ni ya kwanza mkoani Shinyanga akianzia na Kahama.
“Tujipongeze wananchi kutokana na kupata bahati ya wilaya chache zilizotembelewa na kiongozi huyu, Kahama imekuwa mojawapo,” alisema Nkulu.
Alisema
kwa kuwa Jumamosi ni siku ya usafi kitaifa, kila mmoja wilayani humo
ahakikishe anaweka mazingira katika hali ya usafi na kuwaonya
wafanyabiashara kuwa atakayeshindwa kufanya hivyo hataruhusiwa kufungua
biashara.
“Nitafanya
ukaguzi Jumamosi kuhakikisha kila mtu anashiriki usafi. Hilo ni agizo
la kitaifa kwa sasa lazima kila mmoja awajibike, nimewaagiza watendaji
wote wa kata kusimamia hilo,” alisema Nkulu.
Alisema
wananchi watatangaziwa ratiba yote ya Rais Magufuli kwenye gari la
matangazo ambalo litazunguka mji mzima wa Kahama kuwaeleza muda na eneo
ambalo kiongozi huyo atafanyia mkutano.