WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Temeke kuondoa wafanyakazi wa mkataba kwa ili kuwapa ajira ya kudumu kwa wenye sifa na kuwaondoa wasiokuwa na sifa ifikapo Julai 30 mwaka huu.
Amesema kitendo cha kutowaajiri na kuwatumikisha kwa mikataba kwa
muda mrefu kinasababisha wakose stahiki zao jambo ambalo
halikubaliki.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana(Alhamisi, Julai 28, 2016) wakati
akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo na kusisitiza kwamba ni
lazima sula hilo lishughulikiwe haraka kwa sababu hayo ndio matundu
watumishi hewa.
“Mnawatumikisha watu kama vibarua kwa muda mrefu, hapa
kuna wengine wanafanya kazi kwa mikataba kwa miaka mitano hadi sita hii
haikubaliki kwani mnawakosesha stahili zao pale mnapowaachisha kazi,” alisema.
Awali Kaimu Ofisa Utumishi wa Manispaa hiyo Zaitun Hassan alisema
wamekuwa wakitoa ajira za mikataba kwa sababu wamekosa watu wenye sifa
za kuweza kuajiriwa hususan madereva.
“Kwa mara ya mwisho umetangaza lini nafasi za ajira?
Katika mkoa wa Dar es Salaam kweli wanaweza kukosekana madereva wenye
sifa za kuajiriwa? Alihoji Waziri Mkuu.
Zaitun alisema kuwa madereva wengi wanaojitokeza pindi wanapotangaza
ajira wanashindwa kufikia vigezo ikiwemo kuwa na cheti cha VETA na
badala yake wanakuwa na cheti cha kidato cha nne tu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema kuwa kuna wafanyakazi wengine katika
Idara ya Uhasibu na Ujenzi ambao nao wameajiriwa kwa mkataba hivyo
amemtaka Ofisa Utumishi kuomba kibali cha kuajiri kwa Katibu Mkuu
Utumishi.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda kufanya tathmini ya maeneo yote ya shule kwenye
mkoa wake na watakaobainika kuingia katika maeneo hayo waondolewe
haraka.
Alisema baada ya kukamilisha utengenezaji wa madawati kinachofuatia
sasa ni ujenzi wa vyumba vya madarasa, ambapo amezitaka halmashauri
kuweka mipango ya kujenga majengo ya madarasa ya ghorofa ili waweze kuwa
na madarasa mengi katika eneo dogo.
Awali Waziri Mkuu alipokea msaada wa madawati 705 katika hafla
iliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Chamazi wilayani Temeke
ambapo kati yake Ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania umetoa madawati 600
na Jumuia ya Mabohora imetoa madawati 105.
Pia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi
Dk. Agustino Mahiga alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 85
fedha zilizochangwa na watumishi wa wizara hiyo kwa ajili ya kuchangia
utengenezaji wa madawati.
Dk. Mahija alisema watumishi hao walichanga sh. milioni 100 kwa ajili
ya utengenezaji wa madawati ambapo sh. milioni 15 wamekabidhi kwa mkuu
wa wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe ambaye alikuwa mtumishi wa wizara
hiyo ili naye akatengeneze madawati kwa shule za wilayani kwake.
Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini Jaseem Al Najem amesema
Serikali ya Kuwait itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania
katika shughuli zote za maendeleo hususan katika sekta za elimu na afya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM. ALHAMISI, JULAI 28, 2016