![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjninfs33AwRXdUAIGXH-Lc-9k6CgWuy7gSy1PGAkYpTcOGbAICGGOmeDzEWgWeCHqdTzB2ULUajRRofUGLiU7Rk8KtMqQFfz_cPnu-ufDlFlqMZa1AmwPlEfsmBIMULTXr74c9UnXmkALU/s640/1.jpg)
SERIKALI
imebaini ufisadi mkubwa ndani ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA)
kutokana na kukamilika kwa kazi ya Tume iliyoundwa mahususi ili
kuchunguza utendaji wa mamlaka hiyo, na imeagiza kuchukuliwa hatua kwa
watu wote wanaotajwa kuhujumu Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema hayo
wakati akizindua Bodi mpya ya TPA inayoongozwa na Profesa Ignas
Rubaratuka jijini Dar es Salaam jana.
Akiagiza
hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa wahusika waliotajwa katika ufisadi na
ripoti hiyo, alisema kwanza ni baadhi kufikishwa mbele ya Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wengine kuchukuliwa hatua za
kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi lakini akionya kuwa ni marufuku kwa
wahusika kupewa barua za onyo.
Katika
kudhihirisha kukerwa na utendaji wa TPA, Profesa Mbarawa ambaye baadaye
alifanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Bandari ya Dar es Salaam,
aligoma kukabidhi mabegi ya kuwekea nyaraka kwa wajumbe wa Bodi mpya kwa
kusema kuwa yalikuwa ni ya gharama sawa na yale yanayotumika kusafiria
Ulaya.
Akizungumzia
kukamilika kwa kazi ya Tume, Profesa Mbarawa alisema tume hiyo
iliyowajumuisha wataalamu mbalimbali imefanya kazi kubwa ya kuchunguza
utendaji wa TPA na kubaini ufisadi mkubwa katika maeneo mbalimbali
yakiwemo ya mifumo ya miundombinu kama katika mita za kupima mafuta
(flow meters).
Kuhusu
mita za kupimia mafuta, aliitaka bodi hiyo kuwa makini katika kusimamia
utendaji kazi wa mita hizo alizosema serikali imetumia Sh bilioni 12
kuzinunua ili kuhakikisha kuwa zinafanya kazi vizuri na kwamba
zinapoharibika ni lazima uamuzi wa ama kununua mpya au kuzirekebisha
ufanywe haraka.
Alisema
ufisadi mwingine umebainika katika miundombinu ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (Tehama), ambako mingi imewekwa ili kuwanufaisha watu na
si serikali, mgongano mkubwa wa maslahi kwa Bodi ya Zabuni uliochangia
kukwama kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo, ajira za kindugu,
kulindana, mtandao wa wezi, rushwa na uwezo mdogo wa kiutendaji.
Kuhusu
mgongano wa maslahi kwa Bodi ya Zabuni ya TPA, ambayo aliagiza ivunjwe
mara moja na kuundwa mpya, Waziri Profesa Mbarawa alisema Bodi hiyo
imekuwa ikitanguliza mbele kile alichokiita ‘ten percent’ katika kila
zabuni na kukiri wazi kuwa bodi hiyo ni chanzo cha matatizo mengi ya
Mamlaka ya Bandari.
Alisema
kutokana na udhaifu wa Bodi hiyo ya Zabuni, huduma karibu zote
zinazotolewa ndani ya TPA zinatolewa na kampuni ambazo ama ni za
wafanyakazi wa mamlaka hiyo, au za waume au wake zao, na kama si hivyo
basi ni za ndugu, jamaa au marafiki wa wafanyakazi, jambo linalozua
mgongano mkubwa wa kimaslahi.
Kuhusu
ajira, alisema ripoti imebaini viongozi wa TPA wamekuwa wakiwaingiza
kazini ndugu, jamaa na marafiki zao kinyume cha taratibu za utumishi
serikalini na alikwenda mbali kwa kusema kuwa TPA ilipohojiwa kuhusu
kasoro hizo kupitia kwa mwanasheria wake ilisema; “hakuna tatizo,” jibu
alilosema lilimpa mshituko mkubwa.
Kuhusu
mazingira ya rushwa, alimuonya Mwenyekiti wa Bodi hiyo mpya kuwa macho
na rushwa, akisema watu wanaohujumu utendaji wa Mamlaka ya Bandari ni
watu wanaotumia ushawishi wa kiwango cha juu cha rushwa na kutoa siri
kwamba wamewahi kufanya jaribio la kumhonga mjini Mwanza na Dodoma bila
mafanikio.
“Ripoti
imebainisha kuwa wamekuwa wakihonga hata bodi, wanawapa fedha shilingi
milioni tano kwa wajumbe wa bodi na hivyo wanapoteza nguvu ya kusimamia
mambo. Ikitokea hivyo kwa bodi hii, wewe ni Profesa mwenzangu kwa hiyo
ngoma droo lakini nitakuwajibisha. Nitamwomba Rais akuondoe mlango
ulioingilia ndio utatokea na hawa wajumbe ambao wapo katika mamlaka
yangu nitawafukuza papo hapo,” alionya Mbarawa.