![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjtSZYRqJgjxXQoh6AaqSo7T4Y7hyb63lw8PToY_jadMEad6Z9S43_P0Vl0_ozB_Wtzknh8yxQX5UyYQVJqQpSkjCU531tEs5ZnlD53-CXYqdBoHWkJe_dU-asel0dpuVE6mEmAmM-nrLo/s1600/1.jpg)
Jeshi la Polisi mkoani Simiyu limethibitisha kutekwa kwa mgombea ubunge Jimbo la Bariadi, kupitia chama cha ACT Wazalendo Masunga Ng’hozo na watu wasiojulikana.
Akiongea
na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Kamanda wa Polisi mkoani
hapa, Gemini Mushy amesema kuwa tangu kutoweka kwa mgombea huyo, simu
yake imekuwa ikitumika kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa wazazi wake.
Amesema
kuwa ujumbe huo umekuwa ukiwataka wazazi wake kutoa kiasi cha fedha
shilingi milioni mbili na nusu ndipo waweze kumwachia huru vinginevyo
wajiandae kupokea maiti ya mwili wa mtoto wao.
Kamanda
Mushy ameeleza kuwa mgombea ubunge huyo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka
wa tatu katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, (SAUT) kampasi ya
Mbeya alitoweka Septemba 27 mchana akitokea ofisi ya chama hicho mkoa.
Amesema
kuwa jeshi la polisi liliweza kupata taarifa rasmi ya kutekwa mgombea
huyo tarehe 29 Septemba mwaka huu, ambapo ameeleza kuwa mpaka sasa siku
ya nne hajulikani alipo na yuko katika mazingira ya usalama kiasi gani.
“
Ni kweli tumepata taarifa za mgombea ubunge huyo kutekwa na mpaka sasa
ni siku ya nne hatujafahamu yuko sehemu gani na katika mazingira gani
lakini jeshi la polisi kwa kushirikiana na wazazi wake na watu wake wa
karibu tunaendelea kufanya uchunguzi ili tubaini mahali alipo na
wahusika wa tukio hilo” amesema Kamanda Mushy.
Aidha
Kamanda Mushy amesema kuwa kabla ya mgombea huyo kutekwa aliondoka
katika ofisi ya chama hicho Mkoa, alikiwa amebeba begi lake huku akiwa
anaongea na simu huku akimtaka dereva wa gari lake pamoja na fundi
mitambo kumsubiri ofisini hapo.
Kufuatia
tukio hilo Kamanda Mushy ameeleza kuwa jeshi lake linaendelea kufanya
uchunguzi kwa njia ya mitandao ili kubaini ujumbe wa vitisho unatokea
maeneo gani ikiwa pamoja na kuwakamata wahusika wanaoendelea kutumia
simu ya mgombea huyo.
Kwa
upande wake Katibu wa ACT-Wazalendo, Simiyu, Matondo Maduhu
amesikitishwa na kulaani kitendo hicho, hivyo wanaliomba jeshi la polisi
kufanya uchunguzi mapema ili kubaini mahali na kunusuru maisha ya
mgombea huyo.
0 comments:
Chapisha Maoni