Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itaruhusu waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kufika kwenye vituo vya kupigia kura na kufanya mahojiano na wapiga kura pamoja na wasimamizi wa uchaguzi kuhusu zoezi la kupiga kura litakavyokuwa likiendelea.
Hayo
yamesemwa leo na Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima wakati wa mafunzo
ya siku mbili ya waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya
majimbo na wilaya na maafisa wa uchaguzi yaliyofanyika mjini Morogoro.
Mkurugenzi
huyo amesema kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni wa kihistoria kwani kwa mara
ya kwanza waandishi wa habari wataruhusiwa kufika katika vituo vya
uchaguzi kwa lengo la kupata habari kutoka kwa wasimamizi wa uchuguzi na
hata wapiga kura kuhusu namna uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika
Oktoba 25 utakavyokuwa ukiendelea.
Hata
hivyo Kailima amesema kuwa kwa sasa tume inaandaa mwongozo utakaoeleza
taratibu na mipaka ya waandishi wa habari pamoja na watakaohusika kutoa
habari katika vituo hivyo vya kupigia kura.
Katika
hatua nyingine Kailima amesema kuwa NEC imepata taarifa kutoka Mamlaka
ya Hali ya Hewa (TMA) iliyotabiri kuwa mwezi Oktoba kutakuwa na mvua
hivyo NEC imejiandaa kukabiliana na changamoto hiyo.
Hivyo
amewataka wasimamizi wa uchaguzi kubaini mapema maeneo ambayo yanaweza
kuingia maji na kuweka tahadhari ili kuepuka usumbufu kwa wapigakura ama
uharibifu wa vifaa vya kupigia kura zikiwemo karatasi.
0 comments:
Chapisha Maoni