Hakuna shaka kwamba jina la Edward Lowassa (pichani), ndilo linalozungumzwa zaidi kwenye kampeni za urais zinazoendelea sasa;iwe kwa mazuri au mabaya.
Wakati
Chadema na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
vikiendelea kulinadi jina la Lowassa kwa mazuri katika mikutano ya
kampeni, CCM na vyama vingine vimekuwa vikeleza kuwa mgombea huyo wa
Ukawa hafai kuwa Rais.
Mbali
na vyama hivyo, katibu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa naye
amekuwa gumzo katika siku za karibuni, akipinga chama hicho kumkubali
Lowassa kuwa mgombea urais, hali kadhalika, mchambuzi maarufu wa siasa,
Humphrey Polepole ambaye amekuwa akieleza mara kwa mara kuwa Ukawa
imevunja misingi ya kuanzishwa kwake kwa kumpokea Lowassa na kumpa fursa
hiyo.
Anavyotajwa CCM
Kwenye
kampeni za CCM, Lowassa huwa hatajwi na mgombea urais wa chama hicho,
Dk John Magufuli, lakini makada ambao hutangulia kuzungumza kabla yake,
wamekuwa wakiporomosha tuhuma nzito kujaribu kushawishi wananchi kuwa
waziri huyo mkuu wa zamani hafai.
Miongoni
mwa makada hao ni mgombea ubunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ambaye
alidiriki kusema kuwa Lowassa anaweza kushtakiwa wakati wowote kutokana
na kuhusika kwake kwenye sakata la mkataba wa uzalishaji umeme wa
dharura baina ya Serikali na kampuni ya Richmond Development ya
Marekani.
Pia,
katibu mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba amekuwa akieleza udhaifu wa
Lowassa katika mikutano ya hivi karibuni, huku mgombea ubunge wa Mtera,
Livingstone Lusinde akirusha makombora kuhusu hali ya mgombea huyo wa
Ukawa.
Anavyotajwa Ukawa
Lakini
Ukawa na Chadema, ambayo ilijipatia umaarufu kutokana na kupiga vita
ufisadi, wamekuwa wakimtaja Lowassa wakati wakimtetea dhidi ya kashfa za
ufisadi, huku wakimtangaza kwa kutumia msemo wa “Lowassa, mabadiliko;
mabadiliko Lowassa”.
Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ambaye alitangaza kuondoka CCM na
kujiunga na harakati za Ukawa bila ya kutaja chama anachohamia, amekuwa
akijaribu kuwashawishi wananchi kuwa CCM ndiko kuliko na ufisadi mwingi
zaidi ya huo wanaomtuhumu Lowassa, huku akimtetea kuwa katika sakata la
Richmond alifanya hivyo kwa maelekezo ya mkuu wake.
Amekuwa
akijenga hoja yake kwa kutumia ufisadi uliotokea baada ya Lowassa
kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, kama kashfa ya wizi wa fedha kwenye
Akaunti ya EPA, uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow,
utekelezaji mbovu wa Operesheni Tokomeza na uchelewashaji wa malipo ya
makandarasi wa barabara ulioligharimu Taifa Sh900 bilioni.
Maoni ya wadau
Kashfa hizo na kampeni za kumnadi, zimelifanya jina la Lowassa kutajwa zaidi kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
“Ni
kweli viongozi wa CCM wanatumia muda mwingi kumshambulia Lowassa,”
alisema kada wa chama hicho, Aman Ngowi alipoulizwa kuhusu sababu za
jina la waziri mkuu huyo kutamba kwenye karibu mikutano ya vyama vyote.
“Lakini
pia, vyombo vya habari vinachangia. Viongozi wetu kwenye msafara wa
mgombea wa CCM, Dk Magufuli wanaweza kuzungumza mambo mazuri 20, lakini
likitajwa moja tu linalomhusu Lowassa, magazeti yote kesho yake ni
Lowassa,” alisema Ngowi.
Mbunge
wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere na ambaye amekuwa
akisimama kwenye kampeni kumshambulia Lowassa, alisema Tanzania
inakabiliwa na tatizo la ufisadi na rushwa.
Makongoro,
ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, alisema kwa kuwa
ufisadi bado ni tatizo, wataendelea kuwaeleza Watanzania katika kampeni
zao kuwa mgombea huyo wa Chadema ni fisadi.
“Hatuwezi
kunyamaza wakati tunamwona fisadi anaomba nafasi ya urais, ni lazima
tuwaeleze Watanzania kuwa huyo ni mtu hatari kwenu,” alisema.
Alidai viongozi wa Chadema wamenunuliwa ndiyo maana hawakemei tena ufisadi wakati ndiyo walioanza kumwita kwa jina hilo.
Alisema siyo Chadema pekee yao ambao hawazungumzii ufisadi, bali vyama vyote vinavyounda Ukawa.
“Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi wako kimya hawataki kusikia neno ufisadi kwa sababu wamehongwa,” alisema.
Kauli
ya Makongoro iliungwa mkono na Lusinde ambaye alisema kwa kuwa Chadema
hawazungumzii tena ufisadi, CCM wataendelea kuwaambia wananchi kuwa
mgombea huyo ni fisadi.
“Tunayemtafuta
hapa ni Rais, ndiyo maana tunasema tutaendelea kuwaeleza Watanzania
kuwa Lowassa ni fisadi na wasimchague,” alisema.
“Muda
huu ndiyo natoka Bagamoyo kwenye mkutano wa kampeni, nimewaeleza
wananchi kuwa wamwogope Lowassa kama ukoma kwa sababu akichukua nchi
itakuwa ya mafisadi na wala rushwa.”
Lakini,
Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anatetea hali
hiyo akisema ni vigumu wanasiasa kuepuka kutaja udhaifu wa wapinzani
kwenye mikutano yao.
Alisema
Watanzania ni lazima wakubali kwamba katika kipindi hiki cha kampeni,
wagombea watatangaza sera zao, lakini hawawezi kuacha kutaja udhaifu wa
washindani wao
“Ndiyo sababu ya kumtaja Lowassa,” alisema mkuu huyo wa kitengo cha sayansi ya siasa.
“Chadema ndiyo walioanza kumwita Lowassa fisadi na wanachokifanya CCM hivi sasa wanarudia tu. Lakini waasisi wa hilo ni Chadema.
“Unategemea leo CCM wataacha kusema kwenye kampeni kuwa Lowassa ni fisadi wakati kuna ushindani mkali?”
Alisema jambo la muhimu hapo ni matumizi ya lugha yenye staha na vyama kufanya kampeni za kistaarabu.
Lakini
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), anaona
kutajwa huko kwa jina la Lowassa kunatokana na mgombea huyo wa urais wa
Chadema kuwa tishio kwa CCM.
Alisema
kinachotakiwa ni kuwaeleza wananchi sera za vyama vyao ili
kuwashawishi, lakini utaratibu wa siasa za kupakana matope hauna maana
kwa wananchi.
“Kila
siku Lowassa fisadi, hizi ni siasa za majitaka, wananchi wanahitaji
kufahamu mtawafanyia nini endapo mtachaguliwa,” alisema.
Maoni
kama hayo yalitolewa na mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoani Kilimanjaro,
Peter David ambaye alieleza kutofurahishwa na aina hiyo ya kampeni.
Alisema
kampeni zinazofanywa na baadhi ya makada wenzake wa CCM za kuchafuana
majina majukwaani, si nzuri na akataka wanadi sera.
Mkurugenzi
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo - Bisimba
alisema CCM haijiamini, ndiyo maana hivi sasa inazungumzia mtu badala ya
masuala.
“Muda
wote Lowassa fisadi, Lowassa fisadi, watu hawajui vyama vitasimamia
masuala gani. Waache kushughulika na mtu, waeleze hoja, waseme watafanya
nini kama watachaguliwa,” alisema.
“Ukiona wanazungumzia mtu, ujue hali ni ngumu kwao lakini watu wanaojiamini huzungumzia hoja.”
Alisema wagombea kuzungumzia kashfa za ufisadi kila siku badala ya sera, matokeo yake watajikuta wanaangushwa kwenye uchaguzi.
“Watu
wanawapima kwa sera zenu, sasa kama muda mwingi unautumia kuwatuhumu
watu utajikuta huna sera ulizoziuza kwa wananchi,” alisema.
Wakili wa kampuni ya MM Law Chamber, Mohamed Menyanga alikuwa na maoni kama ya Kijo-Bisimba.
“CCM inamwogopa Lowassa ndiyo maana kila wakati inamhusisha na kashfa ya ufisadi wakati haina ushahidi,” alisema Menyanga.
“Muda
mwingi wautumie kuwaeleza wananchi kwa nini ahadi walizozitoa
hawajazitekeleza na siyo kila wakati Lowassa fisadi. Hii haitawasaidia
wananchi,” alisema.
Aliungana
na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Mallya
aliyesema ushindani ni mkali katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ndiyo
maana wagombea wanatumia kila aina ya ‘silaha’ ili kuwashinda washindani
wao.
Alisema wananchi wana haki ya kusikia sera za vyama badala ya kashfa za ufisadi kuanzia mwanzo wa kampeni hadi mwisho.
Wakili
mwingine wa kujitegemea, Carnelius Kariwa wa Dar es Salaam, alisema
anachokiona kwa sasa, kampeni za CCM zinapoteza mwelekeo na malengo.
“Polepole
wameanza kupoteza malengo ya msingi ya kampeni. Lengo la kampeni ni
kuuza sera siyo kuchafuana. Wamelenga mtu badala ya kuangalia nini
Watanzania wanataka.
“Walidhani
wakipiga propaganda dhidi ya Lowassa, Sumaye na makada wa CCM
waliohamia Ukawa wangechafuka lakini wameshindwa kusoma alama za nyakati
nini wanachokitaka Watanzania,” alisema.
Wakili
Kariwa, alikwenda mbali akisema Watanzania walio wengi wanataka
mabadiliko, hivyo hata Dk Magufuli angekuwa anagombea kwa tiketi ya
Ukawa na Lowassa CCM, Dk Magufuli ndiye angeng’ara.
Mawazo
ya Wakili hiyo yanatofautiana na yale ya kada wa ACT – Wazalendo, Buni
Ramole aliyesema CCM imetambua kuwa adui yao mkubwa katika suala la
urais kwa sasa ni Lowassa na ndiyo maana inatumia nguvu kubwa
kumshambulia.
“Kwa
hali ya kawaida, chama kikongwe kama CCM kilichokaa madarakani kwa
miaka zaidi ya 50 hakikupaswa kujinadi kwa kuwasema watu, bali kujinadi
kwa mafanikio wala siyo ahadi tena,” alisema Ramole.
Askofu
Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Jesse Angowi
alisema kitendo cha makada wa CCM kutumia muda mwingi kumshambulia
Lowassa hakimchafui, badala yake kinamng’arisha.
Hata hivyo, Askofu huyo alisema kwa jinsi mwelekeo wa kampeni ulivyo, ni dhahiri rais atatoka ama CCM au Chadema kupitia Ukawa.
Askofu
Angowi alisema haridhishwi na namna CCM ilivyobadili mwelekeo wa
kampeni na kutumia muda mwingi majukwaani kumshambulia Lowassa badala ya
kutumia muda huo kunadi sera zake.
“Lowassa
na Sumaye walikuwa mawaziri wakuu walikuwa wasafi walipokuwa CCM hadi
wakashika nyadhifa hizo. Leo ghafla wamekuwa makapi na kushambuliwa
hivyo?”
Lowassa
amekuwa na nia ya kugombea urais kwa muda mrefu tangu mwaka 1995 wakati
jina lake lilipokatwa. hakuchukua fomu mwaka 2005 wakati Jakaya
Kikwete, aliyekuwa rafiki yake wa karibu, alipogombea.
Lowassa alisema kuwa walikubaliana na Kikwete kwamba waunganishe nguvu ili awamu inayofuata iwe zamu ya mbunge huyo wa Monduli.
Hata
hivyo, mwaka huu jina la Lowassa lilikatwa na ya makada wengine 33, na
ndipo akaamua kujiunga na Chadema kuendeleza ndoto yake ya kuingia
Ikulu.
0 comments:
Chapisha Maoni