Skip to content
test

Jumapili, 9 Agosti 2015

Ni hujuma nzito ndani ya UKAWA



Kinachotokea ndani ya Ukawa, ni matokeo ya mambo makuu matatu; Hujuma toka nje na ndani ya umoja huo, ubinafsi, na uroho wa madaraka.

Matukio ya hivi karibuni ya kujiuzulu kwa viongozi wakuu wawili wa vyama vikuu vya upinzania nchini vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Dk. Wilbroad Slaa na Profesa Ibrahim Lipumba yanaashiria kuwapo kwa hujuma kubwa iliyopangwa mahsusi kuusambaratisha umoja huo, Nipashe limebaini.

Kwa mujibu wa wachambuzi kadhaa wa masuala ya kisiasa nchini waliozungumza na gazeti hili, huku baadhi yao wakigoma kutajwa majina yao wakihofia usalama wao, kinachotokea ndani ya Ukawa, ni matokeo ya mambo makuu matatu; Hujuma toka nje na ndani ya umoja huo, ubinafsi, na uroho wa madaraka.

Ingawa Katibu mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sheriff Hamad, amenukuliwa akisema kwamba kilichojiri katikati ya wiki hii hakitayumbisha umoja huo, duru za ndani zinaonyesha kuwepo hali ya sintofahamu—na hata kusababisha mfululizo wa vikao vya siri—ili kunusuru umoja huo kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu.

Baadhi ya wachambuzi waliozungumza na Nipashe wanaamini kwamba kujiuzulu ghafla kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na kuendelea kuwa ‘mafichoni’ kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ni miongoni mwa ishara zinazojenga mazingira ya kuwapo hujuma hizo.
Chadema na CUF ni vyama vyenye nguvu na mvuto wa kisiasa kati ya vyama vinne vinavyounda Ukawa usiotambulika kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi.

Vyama vingine ambavyo pia vina ushawishi mkubwa kwa umma vikiwa ndani ya Ukawa ni NCCR-Mageuzi, National Convention for Construction and Reform – Mageuzi na National League for Democracy (NLD).

Taarifa za uchunguzi wa kihabari zinathibitisha kuwa matukio ya Profesa Lipumba na Dk Slaa, yana dalili za kuwapo shinikizo la nje ya dhamira na utashi walionao dhidi ya vyama vyao vya siasa.

Tayari kumekuwapo kauli zenye kumbeza Profesa Lipumba kutoka ndani na nje ya CUF, kwamba pamoja na kujiuzulu kuwa ni haki yake, lakini mazingira na sababu alizozitoa havionyeshi kuwapo kwa nia njema dhidi ya chama hicho na Ukawa.

Wote wawili, wameelezewa kuhusika kwa namna tofauti katika masuala yanayotajwa kuwa sababu ya kujiuzulu (Profesa Lipumba) na kutofika ofisi za Chadema (Dk. Slaa), kubwa zaidi likiwa ni ujio wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Profesa Lipumba aliyekuwa Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, alishiriki vikao vilivyoratibiwa na Chadema kwa lengo la kuelezea kusudio la kumpokea Lowassa kuwa mwanachama na hatimaye mgombea Urais anayependekezwa.

Vikao hivyo vya Ukawa vilihudhuriwa na viongozi wa vyama vyote akiwamo Profesa Lipumba anayetajwa kujenga hoja za ushawishi kuhusu nguvu za kisiasa, haki na hitaji la Lowassa kuwa sehemu ya Ukawa.

“Hata ilipokuja hoja ya ufisadi iliyoathiriwa na siasa za chuki kwa makundi ya ndani ya CCM, Profesa Lipumba alijitahidi kumtetea (Lowassa) ndani na nje ya vikao vya Ukawa,” kilieleza chanzo chetu ambacho hata hivyo jina lake tunalihifadhi kwa mujibu wa agizo lake.

Habari zaidi zinaeleza kuwa ingawa kutoweka kwa Dk Slaa kunaweza kuwa na msingi wa kutofautiana na Kamati Kuu ya Chadema kuhusu ujio wa Lowassa, bado kuna mazingira yanayoruhusu watu wakajipenyeza na kunufaika ili hali hiyo iendelee na wao kuzidi kuneemeka.

“Kutokana na msimamo, imani, heshima yake kwa umma na ujasiri wa Dk Slaa, si rahisi kuamini kwamba anaweza kununuliwa aisambaratishe Chadema,” kilieleza chanzo chetu na kuongeza;

“Lakini kuna uwezekano wakawapo watu wanaotumia mbinu chafu kumfanya asirejee Chadema ili waendelee kunufaika pasipo Dk Slaa kuzitambua dhamira zao.” Taarifa kadhaa kupitia vyombo mbali mbali vya habari na mitandao ya kijamii, vimemhusisha mke wa Dk Slaa, Josephine Mushumbusi kuwa nyuma ya tukio hilo.

Hata hivyo, Mushumbusi amekana tuhuma za kumzuia Dk. Slaa kutofika ofisi za Chadema ama kushiriki vikao vya chama hicho.

Gazeti moja linalochapishwa kila siku (sio Nipashe) limemkariri Mushumbusi akielezea masuala tofauti yanayohusu ushiriki wake dhidi ya kutoonekana kwa Dk. Slaa na kusema hakushiriki ama kushirikishwa kufikia uamuzi alioufikia (Slaa).

Lakini taarifa za Uhakika ambazo gazeti hili limezipata Dk. Slaa alishiriki kikamilifu katika vikao vya kumkaribisha Mgombea urais wa Ukawa Edward Lowassa.

Mmoja wa viongozi wa wakuu wa Chadema aliliambia gazeti hili jana, “Dk Slaa alishiriki ipasavyo lakini dakika za mwisho kwa shinikizo la kifamilia toka kwa Mkewe akageuka ghafla”.

Kiongozi huyo ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa vile siyo msemaji rasmi wa chama alisema, “Kilichotokea ni hujuma na wanaotuhujumu wamemfikia Dk Slaa kupitia kwa mkewe…tunazo taarifa za ki-intelijensia kuhusu mawasiliano baina ya mke wa Dk Slaa na mmoja wa mawaziri waandamizi aliyegombea urais katika CCM na kuingia katika hatua ya tano bora (siyo Dk Magufuli).

Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Richard Mbunda, alisema hatua ya Profesa Lipumba inaweza kusababisha mgawanyiko kwa wapinzani walio katika mkakati wa kuunganisha nguvu za kisiasa.

Alisema kimsingi, hakuna sababu ya wapinzani wanaozidi kuaminika kwa jamii, kujiengua ama kujitenga wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Kwa mujibu wa Mbunda, Ukawa inapaswa kujitathimini na kuwaweka sawa viongozi ama wanachama wenye kuonyesha dalili za kutokukubaliana na uamuzi unaofikia kuhusiana na Uchaguzi Mkuu.

“Viongozi wa Ukawa walitakiwa kujua kuwa matukio kama hayo yatajitokeza kwa vile wapo wasioweza kuyamudu mabadiliko,” alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari, alisema Profesa Lipumba amefikia uamuzi unaopaswa kuheshimiwa na umma kumwacha apumzike.

“Kama ilivyo kwangu, nilikuwa mwanachama wa CUF na kwa sasa nipo Chadema. Kwa kuwa amesema anapumzika tumuache tunamtakia kila la heri,” alisema Profesa Safari.

Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) Dk.Helen Kijo-Bisimba alisema Profesa Lipumba ameushangaza umma kwa vile alikuwa mstari wa mbele kufanikisha mambo ambayo baadaye aliyoyakosoa na kujivua uongozi wa CUF.

“Tulimuona akinyoosha mkono na kufurahia sana, sasa alivyokaa hadi dhamira ikamsuta hatuwezi kujua kama kuna watu wamemuuliza maswali ama amehojiwa au kuna watu wamemshawishi…hatuwezi kujua,” alisema.

Hata hivyo, Dk Kijo-Bisimba alisema hatua kama ya Profesa Lipumba inatokea katika siasa ikihusisha zaidi uamuzi binafsi.”

SEIF AIBUKA
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff amesema hatua iliyofikiwa na Profesa Lipumba haitakitikisa wala kukisambaratisha chama hicho.

“CUF ipo kwenye mikono salama na viongozi waliobaki wataendeleza mikakati ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu na kudumisha ushirikiano uliopo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),” alisema.

Maalim Seif alisema hayo usiku wa kuamkia jana kwenye Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, alipowasili akitokea Zanzibar ili kutoa tamko kuhusu kujiuzulu kwa Profesa Lipumba.

Alisema CUF ni taasisi iliyoimarika na kwamba kwa kushirikiana na viongozi, wanachama na wafuasi wake, atatekeleza wajibu wake na kuhakikisha kinapata ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Kauli ya Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ililenga kuwatuliza wanachama walioshutushwa na kujiuzulu kwa Profesa Lipumba juzi.

“Kama ni treni inayokwenda Mwanza ikifika Morogoro abiria watashuka, lakini wengine watapanda, ikifika Kaliua watashuka lakini wengine watapanda…ndivyo ilivyo kwa CUF,“ alisema.

Aliongeza, “waliojiunga CUF kwa sababu ya Profesa wanayo fursa ya kuamua kubaki CUF au kumfuata lakini waliojiunga kwa kufuata malengo ya chama tuendelee kupigania haki sawa kwa wote na mabadiliko ya kweli kwa nchi yetu,” alisema.

KUIDHOOFISHA UKAWA
Taarifa kutoka vyanzo tofauti zinaeleza kuwapo mikakati na mbinu mbalimbali za kutekeleza matukio yatakayohusishwa na mgawanyiko ama kusambaratika kwa Ukawa.

“Ukawa inapozidi kujiimarisha watu wajue kwamba mikakati zaidi ya kuidhoofisha inapangwa ili kama si kusambaratika bado wadhoofike na kutokuwa tishio zaidi kwa watawala katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu,” kilieleza chanzo chetu.

Lakini viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa akiwamo Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, wamesisitiza mara kadhaa kwamba umoja huo hauwezi kudhoofika isipokuwa kuunganisha nguvu zaidi ili kuing’oa CCM kutoka madarakani.

LIPUMBA KUJADILIWA
Maalim Seif alisema chama hicho kitafanya vikao mwishoni mwa wiki hii kujadili kujiuzulu kwa Profesa Lipumba na kumpata mrithi wake.

Akizungumzia hali ilivyo ndani ya Ukawa, Maalim Seif alisema alifanya mazungumzo na viongozi wakuu wenzake wa umoja huo na kuhakikishiwa wataendelea kuwa pamoja.


CHANZO: NIPASHE

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni