Mwenyekiti wa Mdahalo, Ally Mfuruki |
WAGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), juzi
walikimbia mdahalo wa kupambana kwa hoja ulioandaliwa na wenyeviti wa
sekta binafsi na kujulikana kama ‘CEO round table of Tanzania’.
Mdahalo huo ulikuwa na lengo la kujadili mambo makuu mawili, ikiwa ni
sekta ya uchumi na utawala bora na kwa jinsi gani wagombea hao wakipata
ridhaa ya kuliongoza taifa, wangetekeleza vipaumbele hivyo katika
kuliletea taifa maendeleo.
Akizungumza mara baada ya kuahirisha mdahalo huo, Mwenyekiti wa
Mdahalo, Ally Mfuruki alisema amesikitishwa sana na wagombea hao kwa
kushindwa kuhudhuria kwenye mdahalo huo, kwani hadi muda unakaribia wa
kuanza majadiliano, walitoa taarifa za kuhudhuria.
“Nashindwa hata kuelewa ni sababu zipi zimewafanya hawa wagombea
wasifike kwani muda mfupi tu uliopita niliwasiliana nao na wakasema
wanakuja, lakini baada ya kuona muda unaenda na hakuna aliyefika,
nikapata taarifa kuwa hawatafika na sijapewa ni sababu zipi
zimewakwamisha,” alisema Mfuruki.
Waliotarajiwa kuhudhuria mdahalo huo ni Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mawasiliano January Makamba, Balozi
Amina Ally, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri Mkuu
mstaafu, Frederick Sumaye.
Alisema anashangaa kutojitokeza kwao na kuwa aliyejitokeza ni mgombea
mmoja tu, mwanamke pekee katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania kiti
cha urais, ambaye ni Balozi Amina Ally.
Lakini, alithibitisha kupokea taarifa za kutohudhuria kwa Waziri
Nyalandu na kusema kuwa alipata dharura ya kikazi na hivyo alitoa
taarifa ya kutohudhuria mapema na Sumaye pia alipata dharura na kutoa
taarifa ya kutokuwepo kwenye mdahalo.
Kwa upande wake, Balozi Amina Ally alisema anasikitishwa na wagombea
wenzake kwa kutoitika wito wa kuhudhuria, kwani wananchi wanachokitaka
ni kuwafahamu kwa undani wagombea kwa kupitia midahalo na kuweza
kutambua ni yupi atakayewaletea maendeleo na kuwatatulia changamoto
zinazowakabili.
0 comments:
Chapisha Maoni