MKUU
wa Operesheni Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Simon Siro (54)
ametoa ushahidi katika kesi inayowakabili Mwenyekiti wa Chama cha
Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi wake 30 na kudai
mkutano huo ulipigwa marufuku kutokana na taarifa za intelijensia za
kuwapo kwa tishio la ugaidi.
Siro
aliyaeleza hayo juzi mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha, akiwa shahidi wa upande wa mashtaka.
Alidai
Januari 23 mwaka huu walipokea barua ya CUF ikiiarifu polisi kuwa
Januari 27 mwaka huu wangefanya mkutano na maandamano yenye lengo la
kukumbuka watu waliouawa Pemba na kulaani mauaji hayo.
Siro
alisema barua hiyo ya CUF ilidai kuwa chama hicho kimekuwa na tabia
ya kuwakumbuka watu waliouawa na kuyalaani mauaji hayo kila mwaka,
Januari 27.
“Tuliipokea
barua hiyo ya CUF Januari 23, 2015 na Januari 24 na 25, timu ya
intelejensia ilifanya kazi kuona kama yanaweza kufanyika na kumalizika
kwa usalama,” alisema Siro.
Alidai kuwa taarifa hizo za intelejensia zilieleza kuwa lilikuwapo tukio la ugaidi lililokuwa limelenga maandamano hayo.
Siro
alidai pia kuwa kwa kipindi kile yalikuwapo matukio ya unyang’anyi wa
silaha katika vituo mbalimbali vya polisi na kwa sababu hiyo jeshi la
polisi liliyazuia maandamano na mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika,
kwa mujibu wa sheria inayoruhusu kufanya hivyo.
Alidai
polisi hawakuyaruhusu maandamano hayo ya Januari 27, 2001 na
yalikuwa haramu na hata waliouawa hawakuwa wanachama wa CUF pekee bali
hata polisi walikuwamo.
Alidai
jeshi hilo liliandika barua ya kuyapinga yasifanyike na kumkabidhi
Abdul Kambaya kwa niaba ya Katibu wa CUF na walikubaliana kuwa
maandamano na mkutano hautakuwapo.
“Niliamini
kuwa makubalino tuliyofanya Januari 26 yangetekelezwa lakini Januari 27
majira ya saa 8.00 nilipigiwa simu na Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi
wa Temeke, Kamishna Zakaria ambaye aliniambia kuwa walikuwapo watu
wengi wenye mabango katika ofisi ya CUF wilaya ya Temeke.
“Nilimwambia
awaite viongozi waliopo azungumze nao kwa sababu tayari walikuwa na
barua ya katazo lakini baada ya dakika 20 alinipigia simu kuwa wamekaidi
na nilimjibu kuwa sheria ichukue mkondo wake,” alieleza Siro.
Kesi
hiyo inatarajiwa kuendelea Julai 9 na kusikilizwa kwa siku tatu
mfululizo, Julai 29,30 na 31 ambako upande wa mashtaka umeahidi
kuwasilisha mashahidi wengine sita katika siku hizo.
Tukio
la viongozi hao kukamatwa lilitokea Januri 27 mwaka huu wakati
Profesa Lipumba na viongozi wenzake walipokamatwa kwa kuitisha mkutano
wa hadhara kuadhimisha miaka 14 tangu wafuasi wa chama hicho kuuawa kwa
kupigwa risasi na polisi wakati wakiandamana kupinga matokeo ya
uchaguzi wa rais wa Zanzibar mwaka 2001.
Maandamano
hayo ya Januari 27, mwaka huu yalianzia katika ofisi za CUF Temeke
yakiongozwa na Lipumba kuelekea viwanja vya Zakhem kwa ajili ya mkutano
wa hadhara.
0 comments:
Chapisha Maoni