test

Jumatatu, 25 Mei 2015

TAFRANI BURUNDI: Hofu yatanda kuuawa kiongozi wa upinzani




Huku Serikali ikikanusha kuhusika katika mauaji ya kiongozi wa upinzani wa Burundi, baadhi ya makundi ya kisiasa yameanza kuingiwa na wasiwasi kuhusiana na hatima ya kisiasa ya nchi hiyo, wiki moja baada ya Rais Pierre Nkurunziza kusogeza mbele tarehe uchaguzi wa wabunge.

 
Aliyeuawa ni Zedi Feruzi, aliyekuwa mkuu wa Chama cha Umoja wa Amani na Demokrasia (UPD). Aliuawa mwishoni mwa wiki  kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akiwa nyumbani kwake.
 
Mauaji ya kiongozi huyo aliyeuawa pamoja na mlinzi wake, yamechochea hisia za mgawanyiko miongoni mwa wanasiasa ambao wanaendesha shinikizo kumtaka Rais Nkurunziza kutowania muhula mwingine wa tatu wa uongozi.
 
Mwili wa Feruzi ulipatikana nje ya nyumba yake huku watu walioshuhudia wakisema walisikia milio 20 ya risasi kabla ya wahusika wa shambulizi hilo kutoweka kwa gari maalumu waliokuwa wakitumia.
 
Kiongozi mwandamizi wa upinzani, Agathon Rwasa alisema kuwa hakuna taarifa rasmi kuhusu ni nani aliyetekeleza mauaji hayo ingawa alisema kuwa mwanasiasa huyo alikuwa mstari wa mbele kupinga mkakati wa  Rais Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
 
Baada ya Feruzi kuuawa, vijana wa eneo hilo waliandamana na kufunga barabara za mtaa huo kama sehemu ya kuonyesha kutoridhishwa kwao na tukio hilo. 
 
Kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayohatarisha usalama na mshikamano wa taifa ikiwamo maandamano yanayoendelea kushuhudiwa kupinga hatua ya Rais Nkurunziza kuongeza muda wa kutaka kutawala.
 
Zaidi ya watu 20 wamepoteza maisha tangu kuanza kwa vuguvugu la maandamano mwishoni mwa mwezi uliopita.
 
Shambulio la mwanasiasa huyo limetokea siku moja baada ya shambulizi la bomu katika soko moja mjini Bujumbura lililosababisha mauaji ya watu watatu na wengine takriban 40 kujeruhiwa.
 
“Tulisikia milio takriban 20 ya risasi, kila mtu akalala chini, watu waliona gari aina ya Toyota likiondoka kwa kasi,” alisema mkazi wa Ngagara ambaye hata hivyo, hakushuhudia mauaji ya Feruzi.
 
Katika shambulio hilo, ofisa aliyekuwa miongoni mwa waliopewa jukumu la kumlinda kiongozi huyo wa upinzani, alipata majeraha mabaya.
 
“Tulikuwa tunarejea kwa miguu wakati gari aina ya Toyota liliposimama karibu na sisi na wanaume waliokuwa ndani kuanza kutufyatulia risasi,” alisema ofisa mwingine ambaye hakutaja jina lake.
 
Serikali yakanusha
Serikali imekanusha mara moja kuhusika na tukio hilo huku ikisema imeshitushwa na mauaji hayo na kuongeza kuwa kisa hicho kinapaswa kuchunguzwa mara moja ili waliolitekeleza unyama huo wakabiliwe na mkono wa sheria.
 
Polisi imesema inamhoji mtuhumiwa wa shambulio hilo huku ikiwalaumu waandamanaji wanaoipinga serikali kwa kulitekeleza.
 
Huku hayo yakiarifiwa ,kiongozi wa mashirika ya kiraia, Vital Nshimirimana ametupilia mbali madai ya polisi na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchunguza kisa hicho.
 
“Hatujahusika kwa aina yoyote na shambulizi hili, polisi wanajaribu kutupaka matope ili wapate sababu ya kuhalalisha mauaji ya waandamanaji,” alisema Nshimirimana.
 
Majadiliano ya amani yaendelea kwa siri
Katika hatua nyingine, kumekuwa na ripoti juu ya kuanza kwa mazungumzo yanayohusisha pande mbalimbali kwa ajili ya kumaliza mzozo uliojitokeza katika siku za hivi karibuni ambao unahatarisha umoja wa kitaifa.
 
Majadiliano hayo yanayoungwa mkono na jumuiya za kimataifa ikiwamo mataifa jirani, yanaongozwa na Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu, Said Djintit.
 
Wengi wanaamini kuwa majadiliano hayo huenda yakasaidia kutuliza mvutano wa kisaisa unaoendelea  ambao umesababisha maelfu ya raia kukimbia nchi za jirani za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Tanzania.
 
Mgogoro wa kisiasa nchini Burundi ulianza mwishoni mwa Aprili baada ya chama tawala cha CNDD FDD kumteua Rais Nkurunziza kugombea tena katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Juni 26.
 
Mzozo huo ulipanuka zaidi wiki iliopita baada ya Jenerali wa Jeshi, Godefroid Niyombare kutangaza mapinduzi yalioshindwa dhidi ya Serikali ya Nkurunzinza. Kutokana na hali hiyo uchaguzi wa Bunge uliotarajiwa kufanyika Mei 26 umesogezwa mbele na sasa utafanyika Juni 5.
 
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR) limeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi kutokana na ghasia zinazoendelea. Zaidi ya wakimbizi 50,000 wanaripotiwa kuingia nchini tangu kuanza kwa maandamano mwezi uliopita.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni