Na: Mwandishi wetu
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe, amewaasa
Watanzania kuhakikisha wanapambana na viashiria vyote vinavyoweza
kusababisha uvunjifu wa amani na mauaji ya kimbari. Kauli hiyo Dkt.
Mwakyembe ameitoa wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu za mauaji ya
kimbari yaliyotokea nchini Rwanda miaka 24 iliyopita.
Kwenye
hotuba yake Dkt. Mwakyembe amesema mauaji ya kimbari hayatokei ghafla
bali huanza kwa chokochoko na kauli za kichochezi ambazo zina lengo la
kuigawa jamii vipande vipande.
“Kilichotokea
Rwanda ni fundisho kwetu, mauaji ya kimbari hayatakiwi kutokea tena.
Kuhakikisha hayatokei lazima tuyadhibiti mambo yote yanayoweza kuligawa
taifa kwa faida ya kizazi cha leo, kesho na keshokutwa” Dkt. Mwakyembe
alisisitiza.
Kuendelea
kutia mkazo wa ujumbe wake Dkt. Mwakyembe aliinukuu kauli ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, aliyoitoa
wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Rwanda ambapo alisema “haya
hayatatokea tena, hatuwezi kubadili kilichotokea awali, lakini tunaweza
kubadilisha hali ya leo na hata ya baadae”.
Balozi
wa Rwanda nchini mheshimiwa Eugine Kayihura ameishukuru Serikali na
wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kuwa pamoja na Wanyarwanda. Pia
ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kindugu kati ya Tanzania na Rwanda
kwa maendeleo ya watu wake.
Kwa
upande wake Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Alvaro Rodriguez amesema
nchi zote zina wajibu wa kuwalinda wananchi wake dhidi ya mauaji ya
kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu. Pia zinatakiwa
kuhakikisha zinaungana kupambana na mtu au kikundi chochote chenye nia
ya kutekeleza uhalifu kama huo.
Kumbukumbu
za mauaji ya kimbari ya Rwanda huadhimishwa kila mwaka na mwaka huu
maadhimisho hayo kwa Tanzania yamefanyika ukumbi wa mikutano wa Mlimani
City ambapo Dkt. Mwakyembe alikuwa mgeni rasmi. Maadhimisho hayo
yalihudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali wakiwemo mabalozi
wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, watu mashuhuri, viongozi wa
serikali na mashirika ya kimataifa na wanafunzi wa shule za sekondari za
jijini Dar-es-salaam


0 comments:
Chapisha Maoni