Rais
John Magufuli amemtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isaac Kamwelwe na
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge kufuatilia ubadhirifu wa
fedha za mradi wa maji katika Mkoa wa Dodoma na kuhakikisha wahusika
wanakamatwa au maji yanatoka.
Rais
Magufuli ameyasema hayo leo Aprili 27, wilayani Kondoa wakati wa hafla
ya uzinduzi wa barabara ya Dodoma – Babati yenye urefu wa kilomita 251
ambayo ni sehemu ya barabara kuu inayotoka Capetown, Afrika Kusini mpaka
Cairo, Misri.
Ameagiza vyombo vya dola kuwatafuta wahusika wa ubadhirifu wa fedha hizo ambazo amesema ni zaidi ya Sh2 bilioni.
Amesema ni lazima wahusika wachukuliwe hatua kwa sababu hizo ni fedha za wananchi, na ni vyema ziwaletee maendeleo.
“Haiwezekani
tukawa tunaimba maji kila siku halafu maji hayatoki. Vyombo vya dola
vihakikishe wahusika wote wanakamatwa au maji yanatoka. Tukibembelezana
hivi hatutafika, hata hii barabara tusingebana, isingekamilika,” amesema
Rais Magufuli.
Awali
kabla ya Rais Magufuli kuzungumza, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith
Mahenge alisema kuna ubadhirifu wa Sh1.5 bilioni kwenye mradi wa maji
katika wilaya za Kondoa na Chemba ambao mpaka sasa unasuasa.
Mkuu
huyo wa mkoa alisema mradi huo ulitengewa Sh2.8 bilioni kwa ajili ya
wilaya hizo, lakini kulitokea ubadhirifu wa Sh1.5 bilioni.
Amebainisha kwamba vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wa ubadhirifu huo.
0 comments:
Chapisha Maoni