Rais
Dkt. John Pombe Magufuli amezindua ofisi na matawi mawili ya benki ya
NMB Tanzania ambayo imepewa jina la Baba wa Taifa, NMB Kambarage
lililopo jengo jipya la PSPF Dodoma Plaza lililopo mkoani Dodoma.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Rais Magufuli ameipongeza NMB kwa huduma bora ambazo inazitoa na kuitaka kuendelea na kasi hiyo ili kuhakikisha kila Mtanzania anatumia benki kuhifadhi fedha kwani ni sehemu salama.
“Nikiwa
kama mteja na kiongozi wa serikali huwa najisikia vizuri sana kuona
benki hii inazidi kufanikiwa napenda niwahakikishe serikali itaendelea
kushirikiana na NMB.
"Mkurugenzi
wenu ametueleza mambo mengi ambayo mnayafanya mkiwa mmefika kila sehemu
hapa nchini napenda kuwahakikishia kwamba tupo pamoja,” alisema
Magufuli na kuongeza.
“Lakini
Mkurugenzi kwakuwa umekubali kuchagua jina la Kambarage Nyerere
yawezekana ni mbinu nzuri ya kuwavuta wateja wakaja kwa kutambua jina la
Kambarage Nyerere kuwe na uwiano wa huduma zinazotolewa na vitendo vya
Kambarage Nyerere, sitarajii kusikia mtu amekuja alafu akaanza kuombwa
hata rushwa, wote tunajua kuwa Baba wa Taifa alikuwa mpinga rushwa.”
Awali
akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Ineke
Bussemaker alisema benki hiyo kwa sasa imefika maeneo yote nchini na
hivyo kurahisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kwamba wamejipanga
kuendelea kuboresha huduma kwa kushirikiana na serikali.
“Tunafungua
ofisi na matawi mapya mawili katika jengo la PSPF, NMB Kambarage
inalenga kuhudumia wateja wengi ikiwepo wa kawaida na wa serikali na
katika kufanikisha hili tunamshukuru Mama Maria Nyerere kwa kuturuhusu
kutumia jina la mme wake ambaye ni Baba wa Taifa na Rais wa kwanza
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
“NMB
imedhamiria kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma za kifedha, kwa
kutumia matawi, ATM na Wakala kupitia njia ya kidigitali ya intaneti,
apps na simu za mkononi. Kwa sasa NMB ina matawi 218 na zaidi ya ATM 800
nchi nzima,” alisema Bussemaker.
Aidha
Bussemaker alisema pamoja na hilo pia wamekuwa wakitenga asilimia moja
ya faida wanayopata kwa kila mwaka kwa ajili ya kusaidia jamii katika
sekta ya afya, elimu na elimu ya fedha ambapo wamekuwa wakitoa misaada
katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na uhitaji uliopo.
“Tumekuwa
tukitenga asilimia moja ya faida yetu baada ya kulipa kodi kwa ajili ya
Kitengo cha Masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). Kwa mwaka 2017
pekee tulitumia Tsh. 1.4 bilioni ambazo tulisaida shule kwa kutoa
madawati 6,000, kompyuta 300 na vifaa vya maabara,” alisema Bussemaker.
Katika
hafla hiyo benki ya NMB imekabidhi msaada wa Sh. 50 milioni kwa uongozi
wa mkoa wa Dodoma ambazo watazitumia katika shughuli za maendeleo. Hata
hivyo Rais Magufuli ameshauri kuwa mradi ambao pesa hizo zitatumika
upewe jina la NMB.
0 comments:
Chapisha Maoni