Mamlaka
ya Kuzuia Rushwa na Kuhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) inamshikilia ofisa
wa jeshi la polisi kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya zaidi ya
Sh. 250,000.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Ofisa Uhusiano wa ZAECA, Mwanaidi Suleiman
Ally, alisema ofisa huyo Rajabu Juma Simba, mkazi wa Meli Nne-uzi, kwa
kosa la kuomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh. 250,000 kutoka kwa
vijana wawili ambao majina yao yamehifadhiwa.
Alisema
tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 4.30 asubuhi nje ya kituo cha
polisi cha Mwanakwerekwe, baada ya kuwakamata na chombo walichokuwa
nacho aina ya Pasola, kwa kuwatuhumu wanaenda kununua dawa za kulevya
aina ya bangi.
Alidai baada ya kuwapekua hakuwakuta nazo na kuwaamuru kwenda nao kituo cha polisi Mwanakwerekwe kwa mahojiano zaidi.
Alisema
mara baada ya mahojiano, ofisa huyo aliwaamuru vijana hao wampatie Sh.
laki mbili ili awaachie na chombo chao, vijana hao walimpatia shilingi
laki moja na baadae kuwachiwa wao na kuendelea kukushikilia chombo chao.
Kwa
mujibu wa sheria namba moja ya mwaka 2012 ya kuzuiya rushwa na uhujumu
uchumi afande huyo atakuwa amefanya kosa la kuomba na kupokea rushwa
kinyume na kifungu hicho cha sheria.
Alisema uchunguzi wa jalada hilo utakapokamilika litapelekwa kwa Mkurugenzi wa mashtaka kwa hatua za kisheria.
Kamanda
wa Polisi Zanzibar, Muhammed Haji Hassan, alisema jeshi hilo
halitamvumilia askari wake yeyote atakaebainika kujihusisha na vitendo
vya rushwa.
Alisema
jeshi la polisi linafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na sheria zao hivyo
wanapotokea wachache wenye dhamira ya kutaka kulichafua jeshi hilo
ikiwamo kuomba rushwa hawatavumiliwa.
Aliwataka
wananchi kutoa taarifa kwa jeshi hilo au mamlaka husika iwapo
watagundua askari yeyote anajihusisha na rushwa kwa lengo la kuchukuliwa
hatua za kisheria.
Alisema
tabia ya baadhi ya wananchi kukubali kutoa rushwa ni miongoni mwa
vishawishi ambavo wakati mwingine huchangia kutendeka kitendo
alichokiita adui wa haki.


0 comments:
Chapisha Maoni