MZEE Gerald Waya, ambaye ni baba mzazi wa aliyekuwa Msanii
wa Bongo Movies na Model, Agness Gerald ‘Masogange’, amesema mwanaye
alikuwa nguzo kubwa katika maisha yake, hivyo kifo chake ni pigo kubwa
kwake na familia nzima.
Akizungumza nyumbani kwake Mbalizi II wilayani Mbeya, leo
Aprili 22, 2018 Mzee Waya amesema Masogange ni mtoto wanne katika
familia yake ya watoto sita, wa kike wakiwa watano. Amesema Masogange
alisoma Shule ya Msingi Utengule-Mbalizi na sekondari ya Sangu
alikoishia kidato cha pili.
Waya amesema Masogange alipata matatizo hivyo akalazimika
kuacha shule. Hata hivyo amesema hataki kuzungumzia mambo mabaya wakati
huu anapoomboleza kifo cha mwanaye.
“Aliishia form two (kidato cha pili), akapata matatizo
ikabidi aache shule. Tulikosana kidogo lakini tukayamaliza yeye akaenda
Dar es Salaam,” amesema.
Waya amesema, “Mwanangu alikuwa nguvu kwangu, alikarabati
nyumba hii ninayoishi kwa sasa na nilikuwa nafarijika sana, lakini leo
kusikia msiba huu kwa kweli inaniuma sana.”
Amesema Masogange alimpigia simu, “Tukaongea naye
akaniambia ‘mimi baba ninaumwa’. Nikamuuliza nini tatizo akasema, “aah!
baba niombee tu kwa Mungu’. Na Jumamosi iliyopita nilimpigia simu
wakati yupo hospitali kujua maendeleo yake lakini akaniambia ‘baba
byee’. Nikaanza kulia, na hapo sikuwasiliana naye tena hadi nilipopata
taarifa za kifo chake,” amesema.


0 comments:
Chapisha Maoni