Mchekeshaji
maarufu, muigizaji na mshindi wa Shindano la Big Brother Afrika mwaka
2014, Idris Sultan amepata dili la kuwa balozi wa chapa ya kampuni ya
usafiri ya Uber nchini.
Idris
alitangazwa rasmi jana na kampuni hiyo ambapo Meneja Masoko wa Uber
Kanda ya Afrika Mashariki, Elizaberth Njeri amesema kampuni hiyo
ilifanya utafiti kwa miezi kadhaa ili kujua nani anawafaa, na Idris
ameonekana sahihi kwao kutokana na mtindo wake wa maisha.
“Idris
Sultan ni mcheshi, msanii ambaye hafanyi mambo yake kwa mazoea, pia
anaheshimika katika tasnia ya uchekeshaji, tamthilia, na utangazaji wa
vipindi vya redio. Tuna imani kwamba Idris atailetea Uber tija kubwa kwa
sababu yeye anawasiliana na mashabiki wake kupitia mitandao ya jamii
kila wakati,” amesema Njeri.
Kwa
upande wake Idris ameshukuru kwa heshima aliyopewa na kusema amekubali
kuwa balozi wa Uber si kwa kuwa amepata dili ambalo litamlipa, lakini
yeye anaichukulia kama harakati ya kuwakomboa vijana wenzake katika
changamoto ya ajira.
Amesema
Uber isichukuliwe tu kama programu ya kutoa huduma ya usafiri bali
ajira kwa vijana, hata wasomi hawatakiwi kuogopa kuwa washirika wa
huduma hiyo kwa kuogopa kuitwa dereva.
“Kijana
ambaye ana mawazo ya kutafuta, hapaswi kuwa na woga kwamba watu wengine
watamchukuliaje bali kujali ni kiasi gani cha fedha kinaingia na maisha
yako yanakwenda vipi,” amesema Sultan.
Meneja
wa Uber nchini, Alfred Msemo amesema mchango wa Idris Sultan katika
sanaa ya Tanzania unaendana na dhamira ya Uber ya kujenga kampuni ya
kimataifa inayogusa maisha ya madereva na wasafiri wanaotumia mfumo huo
nchini.



0 comments:
Chapisha Maoni