RAIS
mstaafu, Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya
kukusanya fedha kiasi cha Sh. bilioni moja, kwa ajili ya ukarabati wa
Shule ya Sekondari Lindi iliyoungua Julai 2016.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Godfrey Zambi alisema harambee hiyo itafanyika kesho jijini Dar
es Salaam.
Zambi
alisema maandalizi yote kwa ajili ya harambee hiyo yamekamilika na
inatarajia kuhudhuriwa na wadau wa sekta ya elimu nchini.
Alisema
harambee hiyo imepanga kukusanya Sh. bilioni moja ikiwa ni karibu nusu
ya mahitaji ya Sh. bilioni mbili zinazotakiwa kwa ajili ya ukarabati wa
shule hiyo kongwe.
“Kutokana
na fedha tutakazokusanya, tumepanga ujenzi uanze wakati wowote. Zoezi
hili litakwenda sambamba na mpango wa mkoa kuboresha mfumo mzima wa
masuala ya elimu toka ngazi ya awali,” alisema Zambi.
Mkuu
wa mkoa huyo alikiri kuwa mkoa wake ni mmoja kati ya inayofanya vibaya
kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa, lakini akasema hatua
zimechukuliwa kurekebisha, ikiwamo kupima uwezo wa walimu.
Kwa
upande wake, Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Emmy Mchuchuri, alitaja
changamoto zinazoukabili mkoa huo katika kutoa elimu kuwa ni miundombinu
mibovu, uzembe wa walimu, utoro na kutokuwapo kwa chakula cha mchana
shuleni.
Alisema
ofisi yake imeanza kutekeleza maazimio ya wadau juu ya namna bora ya
kuboresha elimu ndani ya mkoa huo, ikiwamo utoaji wa chakula cha mchana
shuleni na mafunzo kwa walimu, ili kujenga uwezo wao wa
ufundishaji.Alisema walimu watakaobainika kuwa na viwango vidogo vya
ufundishaji watashushwa madaraja yao.
0 comments:
Chapisha Maoni