Wanafunzi sita wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamelimwa barua za onyo kwa kuhamasisha maandamano kinyume cha sheria.
Wanafunzi
hao wanadaiwa kuhamasisha maandamano kutaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Mwigulu Nchemba ajiuzulu kutokana na kifo cha mwanafunzi wa Chuo
cha Usafirishaji (NIT), Aquilina Akwilini, aliyeuawa kwa risasi Februari
mwaka huu.
Katika
barua yake ambayo imesainiwa na Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma), Profesa
David Mfinanga, kwenda kwa wanafunzi hao ambao wamekataa majina yao
yasitajwe, imesema onyo hilo ni la mwisho na endapo wataendelea
kujihusisha na vitendo hivyo watasimamishwa masomo mara moja kulingana
na kipengele 14(xi) wakati mashtaka dhidi yake yakiandaliwa na
kushughulikiwa.
“Uongozi
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, umepata taarifa kuwa wewe ni miongoni
mwa wanafunzi wanaojihusisha na vitendo kinyume cha sheria ndogo ndogo
za wanafunzi wa Chuo Kikuu ya mwaka 2011, hususan makosa yaliyoainishwa
kwenye vipengele 4.2(vxiii), 4.2(xix) na 4.2(xxvi).
“Vitendo
hivyo visivyokubalika ni pamoja na kupanga na kuhamasisha maandamano
kinyume cha sheria, kujihusisha na vitendo vinavyokishushia hadhi chuo
kwa kuanzisha kikundi/vikundi visivyoruhusiwa dhidi ya wanafunzi
wenzako, serikali na viongozi wa nchi.
“Kwa
barua hii unatakiwa kuacha mara moja vitendo hivi na endapo utakaidi
utakuwa umejiongezea makosa mengine kama yalivyoainishwa kwenye sheria
ndogo ndogo za wanafunzi wa chuo vipengele vilivyotajwa,” imesema sehemu
ya barua hiyo.
Barua
hiyo pia imetumwa nakala kwa Makamu Mkuu wa Chuo, Naibu Makamu Mkuu wa
Chuo (Taaluma), Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Utafiti), Mwanasheria Mkuu wa
Chuo na Kaimu wa Baraza na Mkurugenzi wa Shahada za Awali kwa
kumbukumbu.
Akizungumzia
barua hiyo, mmoja wa wanafunzi waliopewa barua hiyo amesema barua hizo
wamechukua polisi Kituo cha Chuo Kikuu, baada ya kupigiwa simu Machi 14,
wakitakiwa kuchukua barua hizo lakini hawakuweza kwa sababu walikuwa
wamefunga chuo.
“Kwanza
hatukujua wameandika nini, tulipigiwa simu na polisi wa kituo kicho
kwamba tukachukue barua zetu tulipoenda tukapewa hizo,” amesema
mwanafunzi huyo.
Aidha,
amesema barua hizo zimekosewa kwa sababu wao hawakuhamasisha maandamano
lakini pia sheria hizo ndogo ndogo zinatoa adhabu kama hiyo kwa
mwanafunzi aliyetenda kosa ndani ya chuo.
“Wamekosea
hawajataja tulihamasisha maandamano hayo wapi, sisi hatujawahi kufanya
maandamano ndani ya chuo sheria hizo zinasema endapo mwanafunzi atatenda
kosa ndani ya chuo, hazizui kufanya mwanafunzi kufanya maandamano
kitendo cha kusema sisi tulifanya maandamano si kweli.
“Sisi
tulifanya mkutano na waandishi wa habari tukasema Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi ajipime. Kwa kifupi tumeshachukua hadi kufikia Machi 20,
wote tulikuwa tumeshachukua barua zetu na tumejipanga kuzijibu,”
amesema.
Hata
hivyo, mwanafunzi huyo amesema kuna uwezekani Mwenyekiti wa Mtandai wa
Wanafunzi (TSNP), Abdul Nondo naye yake ilikuwapo isipokuwa imeondolewa
baada ya kusimamishwa masomo kutokana na kesi ya kutoa taarifa za uongo
kwenye mitandao ya kijamii na kudanganya kutekwa inayomkabili.
0 comments:
Chapisha Maoni