Mvutano
wa kisheria katika kesi inayowakabili mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’ na katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,
Emmanuel Masonga umeibuka kwa mawakili wa pande mbili kuhusiana na
ushahidi wa sauti iliyorekodiwa kwa kinasa sauti ambao upande wa Jamhuri
uliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya kuusikiliza na upande wa
utetezi kuupinga.
Mvutano
huo umeibuka baada ya shahidi wa tano upande wa Jamhuri, Inspekta Joram
Magova akiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande kudai kwamba
ndiye aliyefanya kazi ya kurekodi sauti za Sugu na Masonga kwenye
mkutano wao wa Desemba 30 mwaka jana hivyo kuiomba Mahakama kupokea
kifaa kilichotumika kurekodia kama kielelezo cha pili kilichowasilishwa
na shahidi wa wanne, askari Daniel Masanja katika ushahidi unaondelea
kutolewa mahakamani hapo.
Upande
wa utetezi ukiongozwa na mawakili Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu
waliupinga ushahidi huo wakiiomba Mahakama kutoupokea wala kusikiliza
wakidai shahidi aliyetoa kifaa hicho ana masilahi na kesi hiyo hivyo
wanaona ushahidi huo haujakidhi matakwa kisheria.
Hata
hivyo, mawakili wa Serikali, Pande na Baraka Mgaya kwa nyakati tofauti,
waliinuka na kupinga hoja zilizotolewa na mawakili wa utetezi kwa hoja
kwamba walichoiomba mahakama hiyo ni kusikiliza maudhui yaliyomo kwenye
kifaa hicho ambacho kimewasilishwa kama kielelezo na kimepokewa.
“Shahidi
anapaswa kuwa yule aliyeona, kushuhudia na aliyefanya na kusikia. Sasa
hawa wenzetu wanataka kutuaminisha kwamba shahidi siyo yule aliyeona,
aliyesikia na kufanya na kushuhudia, kitu ambacho sicho. Kama kielelezo
kimepokewa na Mahakama hivyo hoja kwamba kisisikilizwe kilichomo ndani
yake, itakuwa imepokea ya nini wakati hatujui kilichomo? Hivyo
mheshimiwa hakimu naomba hoja hii itupiliwe mbali.”
Kifaa
hicho kilitolewa na shahidi wa wanne Masanja ambaye alidai ndiye
aliyekipokea na kukihifadhi katika chumba cha kuhifadhia vielelezo vyote
vinavyotakiwa kutolewa ushahidi mahakamani katika Ofisi ya Upelelezi
Mkoa wa Mbeya (RCO).
Shahidi huyo aliongozwa na wakili wa Mgaya na mahojiano yalikuwa:
Wakili: Shahidi hebu tueleze wewe ni nani na unafanya kazi ofisi gani.
Shahidi: Ni askari polisi nafanyia Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Mbeya (RCO) lakini vilevile ni mtunza vielelezo katika ofisi hiyo.
Wakili: Tangu lini unafanya kazi hiyo?
Shahidi: Tangu mwaka 2004.
Wakili: Vielelezo gani unavyotunza?
Shahidi:
Vielelezo vya kesi inayopelelezwa na kuna aina mbili, kwanza vielelezo
ambavyo vimeshafunguliwa kesi na pili vielelezo ambavyo kesi yake
inakuwa haijafunguliwa mahakamani.
Wakili: Ieleze Mahakama Desemba 30 mwaka jana ulikuwa wapi na ulikuwa unafanya nini?
Shahidi:
Siku hiyo majira ya saa 12 jioni nilikuwa nyumbani lakini nikapigiwa
simu na Inspekta Joram akinihitaji ofisini niweze kupokea vielelezo.
Wakili: Ulifanyeje baada ya hapo?
Shahidi:
Ilinibidi niende na baada ya kufika ofisini nilimkuta Inspekta Joram
akanieleza kuna vielelezo vya kuhifadhi, ametoka kwenye mkutano.
Wakili: Mkutano gani?
Shahidi: Mkutano wa Chadema.
Wakili: Ulifanyika wapi?
Shahidi: Ulifanyika maeneo ya Ruanda Nzovwe.
Wakili: Kielelezo gani ulichopokea?
Shahidi: Ni tape recorder.
Wakili: Baada ya kukueleza hivyo ulifanya nini?
Shahidi: Baada ya kuelezwa hivyo, nikavihifadhi kwa kuvifungia kwenye kasiki ofisini.
Wakili: Hebu ieleze Mahakama, Januari 2 mwaka huu ulikuwa wapi na kufanya nini?
Shahidi:
Nilikuwa ofisini kwangu nikiendelea na majukumu yangu na akaja Inspekta
Joram akihitaji tape recorder ile kwa ajili ya kwenda kuwasikilizishia
viongozi wa Chadema akiwamo mbunge (Sugu).
Wakili: Baada ya hapo nini kiliendelea?
Shahidi:
Inspekta Joram aliendelea na mahojiano na viongozi hao hadi saa nane
mchana akanirudishia kifaa hicho nami nikakihifadhi kwenye kasiki.
Wakili: Tokea siku hiyo ulipokabidhiwa hadi leo (jana) hii nini kiliendelea?
Shahidi: Niliendelea kuhifadhi hadi leo (jana) nilioambiwa vinahitajika mahakamani.
Wakili: Ukiviona unaweza kuvitambua?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Unahitaji Mahakama ifanyie nini vielelezo hivi?
Shahidi: Naomba Mahakama ivipokee kama vielelezo vya ushahidi katika kesi hii.
Wakili: Mheshimiwa Hakimu, shahidi wetu anaomba vidhibiti hivi vyote vipokewe na Mahakama yako kama vielelezo katika kesi hii.
Baada
ya wakili kumuongoza shahidi huyo, Wakili Mwabukusi wa utetezi
alisimama na kuweka pingamizi juu ya kielelezo hicho akipinga kisipokewe
kwa madai kwamba hakijakidhi matakwa ya kisheria na hakina ubora
unaotakiwa.
“Kifaa
kinachotaka kuwa kielelezo mahakamani hapa ni kifaa ambacho
kinasemekana kina maelezo yaliyorekodiwa na mtu mwingine na huyu
aliyerekodi hatujaambiwa alirekodi kwa maudhui gani,” Mahakama
haijaelezwa kwa namna gani ‘data massage’ zilizomo katika kifaa hiki
hazijawa ‘tempered’ na haziwezi kuwa ‘tempered’ kwa namna gani.
Tunapinga kifaa hiki kisipokewe kwa vile hakijakidhi matakwa na hakina
ubora unaotakiwa kisheria.
Baada
ya hoja hizo za Wakili Mwabukusi, Wakili wa Jamhuri, Pande aliinuka na
kusema msingi wa hoja hizo unapinga kutolewa kwa kifaa hicho kama
ushahidi kwa madai kwamba shahidi aliyewasilisha si aliyerekodi kwamba
hawana pingamizi ikiwa kitatolewa na shahidi anayefuata ambaye kimsingi
atakitambua.
Hata hivyo, mawakili wa utetezi walipinga hoja za wakili huyo na kutaka visipokewe vyote
Mabishano
hayo yalidumu kwa takriban nusu saa kabla ya Hakimu Mkazi Mfawidhi,
Michael Mteite kuahirisha kesi hiyo kwa nusu saa ndipo atoe uamuzi juu
ya kinachobishaniwa.
Baada
ya kurejea, Hakimu Mteite alisema Mahakama imejiridhisha kwamba
vielelezo hivyo vinaonekana katika muonekano wake halisi, hivyo
inavipokea kama vidhibiti na itatoa ufafanuzi wa kwa nini iliamua
kuvipokea siku ya hukumu ya kesi yenyewe. Kesi hiyo inaendelea leo.
0 comments:
Chapisha Maoni