Uongozi
wa Kampuni ya uchimbaji madini aina ya tanzanite ya TanzaniteOne Mining
Limited, umejitokeza na kutangaza wazi kuwa wako tayari kushirikiana na
serikali katika kupitia upya makubaliano ya mkataba wa uchimbaji na
kuhakikisha kuwa taifa linanufaika na vito hivyo.
“Wakati
tunasubiri taratibu za serikali kukamilika kabla ya kuanza majadiliano,
tunapenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais John Magufuli na Watanzania kwa
ujumla kwamba sisi kama TanzaniteOne tutatoa ushirikiano utakaowezesha
kuwa na hitimisho lenye tija kwa taifa letu,” ilisema taarifa kutoka kwenye uongozi wa kampuni hiyo.
Taarifa
hiyo rasmi kutoka Bodi ya Uongozi wa TanzaniteOne Limited iliyosainiwa
na Katibu wa Kampuni, Kisaka Mnzava, inasema kuwa viongozi wake wako
tayari kufuata maelekezo yoyote yatakayotolewa na serikali baada ya
mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika baina ya kampuni hiyo na serikali.
“TanzaniteOne
iko tayari kuingia kwenye majadiliano na serikali kwa ajili ya kufanya
mapitio ya mkataba husika pamoja na kurekebisha taratibu zote za
uchimbaji na biashara ya madini nchini kwa manufaa ya Watanzania wote,” alifafanua Mnzava.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo rasmi, TanzaniteOne itashirikiana bega kwa bega
na timu ya serikali itakayoundwa kwa ajili ya kutekeleza wajibu huo,
lengo likiwa ni kuwezesha madini ya tanzanite yanayopatikana Tanzania
peke yake, kuwa yenye manufaa kwa taifa.
“Tunafanya
hivyo kwa sababu mbili: Kwanza ni kutambua juhudi zinazofanywa na Rais
John Magufuli na hatua anazochukua kulinda rasilimali za taifa na
kuhakikisha kuwa madini yanawanufaisha Watanzania wote kwa ujumla.”
“Pili
tunaamini kuwa wabia wa kampuni ya TanzaniteOne, mbao ni Watanzania
wazawa wana wajibu wa kushiriki katika mchakato mzima wa kuliwezesha
taifa kunufaika na rasilimali za madini nchini,” waliongeza viongozi wa TanzaniteOne katika taarifa yao kutoka Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
TanzaniteOne
Mining Limited ni kampuni ya ubia baina ya wafanyabiashara wa jijini
Arusha, Hussein Gonga na Faisal Shahbhat kupitia Sky Associate
wanaomiliki asilimia 50 za hisa na serikali kupitia Shirika la Madini la
Taifa (Stamico) lenye hisa 50 pia.
Wakati
wa ziara yake ya uzinduzi wa Barabara ya KIA-Mirerani, Septemba 27,
mwaka huu, Rais Magufuli aliagiza kupitiwa upya mkataba wa uchimbaji na
biashara ya madini hayo ya vito baina ya Sky Associate na Stamico.
Oktoba
19, mwaka huu, baada ya kushuhudia kutiwa saini makubaliano baada ya
mazungumzo baina ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya uchimbaji dhahabu
ya Barrick Gold Corporation, Rais Magufuli alimuagiza Waziri wa Katiba
na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kwamba timu ya serikali ianze
kufanyia kazi madini ya tanzanite na almasi.
0 comments:
Chapisha Maoni