Mahakama ya Wilaya ya Ilala Oktoba 31,2017 itatoa uamuzi iwapo mshtakiwa Salum Njwete maarufu Scorpion ana kesi ya kujibu au la.
Uamuzi
utatolewa baada ya jana Ijumaa Oktoba 20,2017 upande wa Jamhuri
kufunga ushahidi katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na
kujeruhi ikiwemo kumtoboa macho, Said Mrisho inayomkabili Njwete (34).
Katika
hati ya mashtaka, Njwete anayewakilishwa na wakili Juma Nassoro
anadaiwa kutenda makosa hayo Septemba 6,2016 saa nne usiku eneo la
Buguruni wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Shahidi
wa 10 wa upande wa mashtaka, Salum Masoud mkazi wa Buguruni ambaye ni
mfanyabiashara wa kuuza chenji katika kituo cha daladala amedai siku ya
tukio alikuwa katika biashara zake.
Akiongozwa
na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi, Flora
Haule alidai akiwa katika shughuli zake alishuhudia mabishano kati ya
mshtakiwa na mteja aliyekuwa akinunua bidhaa eneo hilo.
Amedai alimuona mshtakiwa akigonga meza akimlazimisha mteja huyo kumfuata.
Shahidi huyo alidai mteja huyo alishangaa kuitwa na mtu asiyemfahamu hivyo alikataa kwenda.
Masoud
alidai alimuona mshtakiwa akimfuata mteja huyo, kumvuta, kumwangusha
chini na kuanza kumpiga maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Amedai
alimwona mshtakiwa akichomoa kisu na kumtoboa mteja huyo na alisikia
sauti ya kilio chake cha kuomba msaada, huku akitokwa damu maeneo
mbalimbali ya mwili wake.
Shahidi
huyo alidai mshtakiwa alichukua mkufu aliokuwa amevaa mteja huyo
shingoni na uliokuwa mkononi. Pia, alidai alichukua pochi iliyokuwa
mfukoni na alimsukuma kwenye Barabara ya Mandela ambako alianguka.
Baada ya mshtakiwa kuondoka, Masoud anadai walimnyanyua mteja huyo na kumweka eneo la wazi linalotenganisha barabara.
Amedai
mtu aliyekuwa eneo hilo alitoa taarifa polisi ambao walifika eneo hilo
na kuwatawanya kabla ya kumchukua majeruhi na kumpeleka hospitali.
0 comments:
Chapisha Maoni