Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amemponda aliyekuwa
Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu akisema walishamweka
pembeni kwa kuwa hakuwa mtu wa muhimu kwao.
Akizungumza
jana Jumatatu usiku katika kipindi cha Msemakweli kinachorushwa na
Channel Ten, Polepole aliyekuwa akizungumzia mafanikio ya Rais John
Magufuli kwa kipindi cha miaka miwili, alimtakia heri Nyalandu huku pia
akisema amejimaliza mwenyewe.
“Ameondoka
mwanachama mmoja wa CCM leo (jana) amekwenda upinzani. Katiba yetu hii
ya Jamhuri ya Muungano inasema kila mtu ana uhuru wa kujiunga na chama
chochote. Tunaheshimu uamuzi wake, tunamkatia heri katika chama
anakokwenda,” alisema Polepole.
“Aliyeondoka
leo ni ‘very insignificant’ yaani kwa Kiswahili hatujaona utofauti.
Ndiyo maana sisi tumetoa maelekezo kwa Serikali kwamba, watu ambao
hawakuweza kutukimbiza katika awamu ya tano kwenye maendeleo ya Taifa
letu kwenye uongozi wa awamu ya tano wawekwe benchi kwanza. Sasa
wamewekwa benchi,” alisema Polepole.
Hata
hivyo alisema Nyalandu ana haki ya kikatiba kuamua kwenda chama
chochote anachokitaka na kwa kuwa CCM ni chama cha kidemokrasia
hakitamlazimisha kubaki.
“Chama chetu kina watu wengi wakongwe na wa muda mrefu na kitaendelea kuwepo na kinafanya kazi watu wanaona,” alisema.
Alisema kwa kuwa Nyalandu alishawekwa benchi alipaswa ajitafakari na kujipanga upya.
“Unajua
unapowekwa benchi uelewe kwamba ama uongeze mazoezi au umeongezeka kilo
mbio zako zimepungua, kwa hiyo tunakuweka benchi ujitafakari kwamba
hauna msaada kwenye timu,” alisema na kuongeza:
“Sasa
ukiwekwa benchi kwa muda mrefu ukapata timu ya mchangani, wanacheza
chandimu, wewe unafahamu chandimu? Unatoka daraja la kwanza unakwenda
daraja la nne na ndiyo chandimu na ndiyo umekwenda na maji.”
Aliendelea
kujisifu akisema CCM haina wasiwasi kwa kuwa kiwango chake ni cha juu
na wachezaji wake ni wa kimataifa na wametengenezwa vizuri kuwahudumia
Watanzania.
Huku
akipekua katiba ya CCM, Polepole alimsikitikia Nyalandu akisema
anakwenda kwenye chama kisicho na itikadi akiacha CCM yenye itikadi ya
ujamaa na kujitegemea.
“Unamtazama
mtu amekwenda kutafuta itikadi pahala ambapo kuna itikadi
isiyojulikana. CCM itikadi yetu ni nini? Ibara ya nne, ibara ndogo ya
tatu, anakwambia itikadi ya CCM ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee
ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru,” alisema na kuongeza:
“Sisi
ni wajamaa kwa maneno na kwa matendo. Uliza chama anachokwenda itikadi
yao ni nini? Kuna malango ya mbinguni na malango ya jehanam. Sisi
tunamtakia mafanikio mema.”
0 comments:
Chapisha Maoni