Ofisa
Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jennifer Mushi
amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na
mashitaka mawili ikiwamo la kumiliki magari 19 na kuishi maisha ya
kifahari kuliko kipato chake.
Mushi
alifikishwa mahakamani hapo jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,
Huruma Shaidi.
Akisoma
mashitaka hayo, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Vitalis Peter alidai
kati ya Machi 21, mwaka jana na Juni 30, mwaka jana katika maeneo
tofauti ya Jiji la Dar es Salaam, akiwa mwajiriwa wa TRA, mshitakiwa
huyo alikutwa akimiliki magari 19 ambayo ni mali zisizolingana na kipato
chake.
Alitaja
magari hayo kuwa ni Toyota Rav 4, Toyota Dyna Truck, Toyota Vitz,
Suzuki Carry, Toyota Ipsum, Toyota Wish, Toyota Mark ll, Toyota
Regiusage, Toyota Estima, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota
Hiace, Toyota Estima, Toyota Lasso, Suzuki Carry, yote yakiwa na
thamani ya Sh 197, 601,207.
Katika
mashitaka ya pili, inadaiwa kuwa kati ya Machi 21,2012 na Machi 30,
mwaka jana, Dar es Salaam akiwa mwajiriwa wa TRA aliishi maisha ya
kipato cha juu tofauti ya thamani ya Sh 333, 255,556, tofauti na kipato
chake.
Mshitakiwa
alikana mashitaka hayo na upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi
hiyo, umekamilika na kuomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili
ya kuanza kusikilizwa maelezo ya awali.
Hata
hivyo, Wakili wa Utetezi, Elisalia Mosha aliomba mahakama hiyo kumpatia
dhamana mteja wake kwa sababu mashitaka aliyonayo yanadhaminika
kisheria.
Hakimu
Shaidi alimtaka mshitakiwa huyo kuwa na mdhamini mmoja, atakayesaini
bondi ya milioni 20 na mshitakiwa alikidhi masharti ya dhamana.
0 comments:
Chapisha Maoni