test

Ijumaa, 2 Juni 2017

Mjadala wa BANGI Watikisa Bunge


Leo wakati mkutano wa saba , kikao cha 40 kikiendela bungeni Dodoma umeibuka mjadala wa dawa za kulevya aina bangi baada ya baadhi ya wabunge kusema kuna vitendo vinavyofanywa na baadhi ya polisi nchini vinatokana na polisi hao kuwa wamelewa bangi.

Katika mjadala huo Mh Spika Job Ndugai naye alichomekea kuwa huwa anasikia watu wanasema bangi zinaongeza nguvu, hivyo naye alitaka kujua hizo bangi zinaongeza nguvu za aina gani, huki akiwauliza wabunge ambao wanatokea maeneo ambayo bangi imekuwa ikiripotiwa sana.

Kufuatia mjadala huo kuendelea alisimama Mbunge Esther Matiko Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara na kusema yeye mwenyewe huwa anaona polisi wakichoma bangi katika maeneo hayo na kudai huenda baadhi ya vitendo vinavyofanywa na polisi wetu ni kutokana na kuathirika na moshi wa bangi wakiwa wanachoma bangi hizo. Lakini katika ufafanuzi wa Naibu Waziri wa Afya alisema polisi hao wao huwa hawaathiriki na moshi huo.

"Jamani tunapojadili juu ya suala la madawa ya kulevya si jambo la mzaha, ni kwamba polisi wanapokwenda kuchoma bangi mashambani huwa wanajifunika vifaa maalum lakini hata kama hawajifuniki vifaa hivyo bado ile bangi ikiingia kwenye miili yao itaondoka ndani ya siku 30 kwani inageuka na kuwa chumvi na kutoka kwa njia ya mkojo na jasho. Lakini kwa watu ambao wanatumia kila siku yaani leo, kesho, kesho kutwa na kuendelea wao wanakuwa ni clonic wa dawa hizo" alisema Kigwangalla

Licha ya Naibu Waziri wa Afya kutoa ufafanuzi juu ya uchomaji wa bangi lakini Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Joakim Mhagama alisimama na kutoa ufafanuzi wake pia akisema kuwa polisi hawajaathirika na bangi kutokana na namna ambavyo huwa wanachoma bangi hizo kwa kufuata utaratibu mzuri.

"Mh. Spika vikosi vya polisi vinavyofanya utekeketezaji wa bangi, zipo njia nyingi wanatumia kuteketeza bangi hizo, kwanza wakiwa wanafanya zoezi hilo huwa wanaangalia uelekeo wa upepo lakini pia maandalizi mengine ya vifaa vyao vya uteketezaji wa bangi, aina ya mafuta yanayotumia kwenye kuchomea bangi hizo vinawafanya kuwa salama kabisa, kwa hiyo siyo kweli kwamba likitokea tatizo kwenye jeshi la polisi kwamba polisi wetu wameathirika na matumizi ya bangi, kwani polisi wetu ni weledi na wanafanya kazi kwa kufuata utaratibu na sheria" alisisitiza Mhagama

Kwa kumalizia mjadala huo Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kuwa nchi nzima na viongozi wamesikia juu ya jambo hilo hivyo wanapaswa kuwa makini katika utekelezaji wa mambo hayo.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni