test

Jumatatu, 5 Juni 2017

Makamu wa Rais: Wasiopeleka michango ya wanachama kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii wachukuliwe hatua


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewaagiza waajira wasiopeleka au kuchelewesha michango ya wanachama kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii nchini wachukuliwe hatua za kisheria ili kukomesha tabia hiyo.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo 3-June-2017 Jijini Mwanza wakati anafungua semina ya maisha baada ya kustaafu,fursa ya mafao,uwekezaji iliyoandaliwa na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) kwa ajili ya wastaafu watarajiwa 450 kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa waajiri wakichangia kwa mujibu wa sheria kwenye mifuko hiyo watawezesha wanachama wao kupata mafao kikamilifu na kwa wakati.

Kuhusu madeni ya Serikali kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini, Makamu wa Rais aliwahakikishia Wakurugenzi wa mifuko hiyo kuwa Serikali inashughulikia madeni hayo na baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa madeni hayo basi malipo yatafanyika haraka iwezekanavyo.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha michango ya pensheni kwa wafanyakazi wa taasisi zinazopata ruzuku kutoka Serikalini inalipwa kwenye mifuko hiyo kwa wakati.

Aidha, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan aliwahimiza wastaafu watarajiwa kote nchini waache tabia ya kukata tamaa baada ya kustaafu bali wajipange vyema na kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo viwanda vidogo, kilimo na biashara.

Alisema kuwa kama wastaafu hao watawekeza katika maeneo hayo watatoa ajira kubwa kwa vijana badala ya kutumia mafao yao kwenye matumizi yasiyo ya lazima.

“Wazee ni rasilimali na hazina kubwa kwa taifa kama waswahili wasemavyo panapo wazee hapaharibiki jambo hivyo basi ni matumaini yangu kuwa mfuko wa PSPF mtaendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu kuhakikisha kuwa hazina hii ya wazee wetu wanapata haki zao kwa mujihu wa sheria za nchi pale wanapohitaji huduma toka kwenu.”Alisisitiza Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan alionya wastaafu hao watarajiwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima bali watumie fedha watakazopata katika shughuli za kiuchumi kwa ajili ya maslahi yao ya baadaye.

Makamu wa Rais pia alipongeza jitihada zinazofanywa na mfuko wa PSPF kwa kutoa mafunzo kwa wastaafu watarajiwa kwa ajili ya kuwasaidia kujipanga vyema pindi watakapostaafu utumishi wao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Ashatu Kijaji aliwahakikishia wastaafu hao watarajiwa kuwa wa mkoa wa Mwanza kuwa Serikali itaendelea kusimamia vyema mifuko ya hifadhi ya jamii ili iweze kutoa mafao bora na kwa wakati.

Dkt Ashatu Kijaji pia alihimiza wastaafu hao watarajiwa kutumia vizuri mafao wanayopata kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni