test

Jumatatu, 5 Juni 2017

Meck Sadiki atoa ya moyoni uteuzi wa Mgwira


ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki amesema uteuzi aliyoufanya Rais John Magufuli kwa kiongozi wa Chama cha ATC Wazalendo, Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ni sahihi.
Sadiki aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa, Rais hajakosea kumteua Mghwira kuwa kiongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kwani mwana mama huyo ni mchapakazi, mzalendo na asiye na ubaguzi, na uongozi unahitaji mtu wa aina hiyo. “Nilimfuatilia Mghwira katika kampeni zake akiomba urais, ni mwanamke mtulivu, mwenye mtazamo wa maendeleo na mkoa huu wa Kilimanjaro unataka mtu atayetazama watu kwa maendeleo na si kwa vyama,” alisema Sadiki.
Alisema kuna maeneo matano ambayo angependa mteuliwa huyo ayape kipaumbele ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji. Alisema kama mazingira yataharibiwa zaidi ndani ya miaka 10 mkoa utakuwa jangwa na na kukumbwa na baa la njaa. Katika eneo hilo, alitaka Mghwira ashirikiane na taasisi na viongozi wengine kutunza mazingira na vyanzo vya maji.
Eneo jingine ni uvushwaji wa bidhaa za magendo kutoka Tanzania kwenda Kenya. Alisema mkoa unakosa mapato mengi kutokana na mbinu za ujanja za wafanyabiashara wasio waaminifu. Alimtaka kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kujipanga vyema kudhibiti hilo. Dawa za kulevya Alisema kuwa zimekuwa zikiathiri maendeleo ya mkoa.
Akatolea mfano Same ambako mirungi inalimwa sana na kumtaka alishughulikie huku akiwataka wananchi kumpa ushirikiano kuwafichua wanaofanya biashara hiyo haramu. Mimba mashuleni Alieleza kuwa mwishoni mwa mwaka jana hadi Februari mwaka huu wamepatikana wanafunzi 38 wenye mimba kwenye wilaya ya Same pekee. Amesema kwa kuwa mama Mghwira ni mwanamke, anayo nafasi ya kuzungumza kwa ndani na mabinti na wanawake wasikatishe masomo.
Siasa Alisema kuwa mtu akiwa nje ya mkoa wa Kilimanjaro anaweza akawa na mtazamo hasi wa siasa za Kilimanjaro, ila hilo si tishio kwani anaamini kuwa kiongozi kwenye mkoa huo anashirikiana na wananchi na maendeleo yanapatika. ACT inasemaje Wakati Sadiki akiwa alishaachia ngazi hiyo na Rais tayari ameshamtangazia uteuzi wa nafasi hiyo mama Mghwira, Chama cha ACT Wazalendo kimesema hatua ya Rais Magufuli kuwateua viongozi wa chama hicho kushika nyadhifa mbalimbali katika utawala wake ni kuonesha kuwa chama hicho kina watu wenye uwezo wa kufanya kazi nzuri na upinzani wana uwezo vile vile.
Hata hivyo, kimesema uteuzi wa Rais kwa Mwenyekiti wa chama hicho Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ni pigo kwa chama hicho kwani bado kilikuwa kinamhitaji. Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu alisema, “Kwetu tumepoteza hatuwezi kusema tunafurahia uteuzi huu kwa sababu huwezi kumpa mtu keki yako unayoipenda na wewe ukabaki na keki,” alisema Ado.
Alisema kuteuliwa kwa mwenyekiti wao kuwa mkuu wa mkoa ni changamoto kwa chama kwani ni kiongozi wa ngazi ya juu ambaye anategemewa kuendelea kukijenga chama. “Jambo hili lina sura mbili, kama Mghwira tunamuachia mwenyewe atakuja kuliongelea ni jambo binafsi, “ alisema Ado. Hata hivyo alisema Kiongozi wa chama hicho, Kabwe Zitto aliwahi kusema bungeni kuwa katika nchi zinazoendelea
kufanya kazi serikalini ni jambo ambalo linatakiwa kufanywa na Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao ili mradi uwe na uwezo.
“Pengine Rais ameanza kufahamu kuwa hata upinzani wana uwezo wa kulitumikia taifa hili katika ngazi za uongozi, hata hivyo mwenyekiti wetu sasa anachukua majukumu mapya sasa hatuwezi kumtumia kama awali katika chama chetu, “ alisema. Ado alisema hata hivyo chama kinamsubiri mwenyekiti wao huyo ambaye anatakiwa kufanya maamuzi aidha kupokea uteuzi huo au la.
Alisema chama cha siasa chochote kina malengo yake ni kushika dola na kuongoza kwa ilani na namna ambavyo wanaona inafaa tofauti na sasa Mghwira ataongoza kwa matakwa ya Chama Cha Mapinduzi kilichomteua. “Hata kama mama atakuwa kiongozi sasa hawezi kutekeleza ilani ya ACT, kwa hiyo hatuwezi kusema kama uteuzi huu ndani ya chama umetufurahisha,” alisema Ado.
Alipotafutwa Mghwira hakupatikana ambapo ilielezwa kuwa yuko nje ya nchi na anatarajiwa kurudi leo na kiongozi wa chama hicho, Zitto alisema hajawa na muda wa kuzungumza katika jambo hilo. Hata hivyo, jana jioni kupitia kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii (Facebook), Zitto aliandika, “Nimekuwa naulizwa sana kuhusu uteuzi wa mwenyekiti wa chama chetu kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Nimekuwa kimya kwa sababu tumepokea taarifa za uteuzi huo kutoka katika vyombo vya habari. Mwenyekiti yuko nje ya nchi na kutokana na tofauti za saa hatujawasiliana naye. Tutatoa tamko kamili atakapokuwa amerejea nchini… “…Ninawataka wanachama wote wa ACT Wazalendo wawe watulivu na kama kuna masuala yanayohusu maamuzi ya vikao vya chama tutawajulisha.
“ Aliyeteuliwa ni Mwenyekiti wa chama Taifa, sio mshauri au mwanachama tu. Ni mmoja wa viongozi wa juu wa Chama chetu. Uteuzi wake unahitaji kikao cha kamati kuu ya chama kukaa na kujadili. Nitaweza kutoa taarifa baada ya vikao vya kamati Kuu. Kwa sasa umma usubiri vikao Kwa mujibu wa Katiba ya Chama chetu.” Juzi Rais Magufuli alimteua Mghwira kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro kushika nafasi ikiyoachwa wazi na Said Meck Sadick ambaye alijiuzulu wadhifa huo. Mbali na Mghwira, kiongozi mwingine wa chama hicho aliyeteuliwa na Rais ni Profesa Kitila Mkumbo aliyeteuliwa Aprili 4 mwaka huu, kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni