Hivi
karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe
Magufuli alipokea ripoti ya Kamati ya kwanza na ya pili ya uchunguzi wa
makontena 277 ya mchanga wa madini (makinikia) yaliyokuwa njiani
kusafirishwa nje ya nchi na uchunguzi ulifanyika na kulibaini ndani ya
mchanga huo kuna dhahabu na madini mengine kwa asilimia kubwa.
Aidha, Mhe Rais amechukua hatua mbalimbali kulingana na ushauri wa kamati husika, pamoja na maamuzi yake kama Rais.
Kutokana
na sakata la hilo, Idara ya Habari-MAELEZO imepata fursa ya kufanya
mahojiano na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mstaafu Mheshimiwa, Jaji Joseph Sinde Warioba
katika ofisi zake zilizopo Osterbay Jijini Dar-es-salaam.
SWALI:
Ninanukuu maneno ya Baba wa Tafa, Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere
kuhusu raslimali za nchi na hususan madini alisema: “Madini yetu
tuliyonayo ni vema kuyaacha mpaka Watanzania watakapokuwa na ufahamu wa
kutosha wataamua kuyachimba” mwisho wa kunukuu nini maana yake?
JIBU: Mara
baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 Hayati, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere alipokea nchi kama Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika
huru akiwa hana wataalamu zaidi ya madaktari 2 na yeye mwenyewe ambaye
alikuwa msomi kutoka chuo Kikuu cha Edinburg Uingereza. Kwa hali hiyo,
Mwalimu alikuwa sahihi usingeweza kuruhusu rasilimali za nchi mfano
madini kuchibwa na wageni kutoka nje maana yake Watanganyika wangekuwa
watazamaji tu bila kufaidika na lolote.
Mwalimu
alihakikisha anawekeza katika elimu ambayo ilikuwa bure kuanzia msingi
hadi chuo kikuu elimu ndio msingi wa kuondoa Ujinga Umasikini na
Maradhi. Alitambua Watanganyika wakielimika na kupata utaalamu wa madini
ikiwani pamoja na uchimbaji watakuja kuyachimba na kufaidika.
SWALI:Tanzania
ni kati ya nchi zilizobarikiwa kuwa na raslimali nyingi za kila aina
kuanzia madini, gesi, wanyamapori na hifadhi, misitu, milima, maporomoko
ya maji, mabonde maziwa makubwa kwa madogo, bahari ya hindi na
raslimali za mazao ya uvuvi, nchi yenye ardhi ya kutosha watanzania
wenye uwezo wa kufanyakazi kwa ufanisi . Unadhani nini tatizo letu, nini
cha kufanya?
JIBU: Sioni
kama kuna tatizo la msingi lakini, ni suala la uelewa mara nyingi kuna
watu ambao huamini viongozi wao kwa kila kitu wanachosema. Lazima
wananchi wawe makini kwa sababu tatizo la watanzania ni maendeleo kila
mwananchi ana kiu ya kutaka tufikie mahala pazuri kama Taifa na mimi
nakubaliana nao kabisa.
Tuna
rasilimali nyingi, ambazo kimsingi tukiweza kuzishughulikia kwa makini
kama lilivyoshughulikiwa suala la mchanga wa madini tutakuwa mbali sana
kiuchumi.
Mosi,
tuangalie rasilimali ya madini kwa mapana yake na kushughulikia
wawekezaji wa ndani na wale wa nje, Barick na Acaccia ni sehemu ndogo
sana ya madini, tuangalie wachimaji wa ndani mfano Tanzanite ni aibu
madini yanachimbwa Manyara biashara hii inatokaje Mererani na kufanyika
Nairobi na New Delhi tujiulize kwa nini sio Arusha na Dar-Es-Salam.
Pili,
upande wa rasilimali za maziwa makubwa tuliyonayo Victoria, Tanganyika
na Nyasa, Bahari ya Hindi kuanzia Moa mpaka Tanga kwa kiasi gani
tumeweza kutumia rasilimali za bahari maharamia wanakuja na meli zao
wanavuna tu na kuwatajirisha watu wengine. Mfano ziwa Victoria
linategemewa na wananchi wengi na sasa samaki hamna wamekwisha kwa
sababu hatusimamii rasilimali zetu ipasavyo. Maana suala sio kuvuna tu
tunalindaje hizi rasilimali zetu ili ziwepo leo kesho na vizazi vijavyo.
Tatu,
Maliasili zetu za wanayamapori, mbuga za wanyama, vitalu vya utalii
unampaje mfanyabiashara kibali cha kuwinda miaka 99 yaani atumie yeye,
wanawe na wajukuu zake, watanzania watatumia lini, haya ni masuala ya
msingi kabisa ya kuangalia upya.
Nne,
Ardhi Mwalimu alisema ili tuendelee tunahitaji vitu vine Watu, Ardhi
Siasa Safi na Uongozi Bora. Mwalimu Nyerere aliona ardhi ndio kilakitu
hivyo vyote tulivyovitaja vipo ardhini pamoja na sisi wanadamu
tunaitegemea kwa kila kitu. Maeneo mengi yaliyotumiwa na watu kwa
shughuli za ufugaji aidha , yana matumizi mengine kama nyumba, kilimo
cha mashamba makubwa, na idadi ya watu inaongezeka ardhi ni ileile hii
imesababisha migogoro ya watumiaji wa asili wa maeneo hayo na wenye
matumizi mengine tunatatuaje changamoto hii.
SWALI:
Kwa kuwa umebobea katika masuala ya mikataba na sheria, ushauri gani
unautoa katika masuala yote ya raslimali za Tanzania? Nani anatakiwa
kusimamia raslimali hizi kwa ufanisi?
JIBU: Hii
sio suala la mjua sheria au asiyejua, Mwanasheria lazima anazijua
sheria ndio maana amepewa dhamana. Linalojitokeza ni ukosefu wa maadili
ya uongozi, imani, utiii, uwazi na kutopenda nchi yako na Watanzania
ambao wamekupa dhamana ya kusimamia jambo.
Ndio
maana Mwalimu Nyerere aliweka miiko ya uongozi, maadili ya uongozi
kwenye Azimio la Arusha. Kila mwananchi alikuwa anaweza kujua kiongozi
huyu muadilifu au sio muadilifu na anachukuliwa hatua kabla mambo
hayajaharibika.
Lakini
sio vema kumhukumu mtu kwa jambo lolote lile, ni vema busara itumike
kujua kilichotokea mfano hili suala la mchanga wa madini ya makinikia.
Jambo
la msingi ni kutafuta suluhu itakayotupeleka mbele, tuone sera zetu
zikoje na zinatusaidiaje kulinda rasilimali za Taifa, tunarekebisha vipi
kuondoa tatizo, sheria na utendaji kwa ujumla. Naomba watanzania tutoe
maoni na mawazo yatakayoboresha sera, sheria na utendaji au usimamizi wa
rasilimali husika. Tunaweza kurudisha miiko na maadili ya uongozi
katika kusimamia rasilimali za nchi, kila Mtanzania ajue sio mali yake
ni ya Watanzania wote lazima aitunze vinginevyo atahukumiwa kwa hilo.
SWALI: Ni
ukweli usiopingika kuwa kosa limeshafanyika kwa hili tuliloliona la
mchanga wenye madini ya dhahabu, ambapo mhusika ambaye ni mmiliki wa
Kampuni inayobeba mchanga huo tangu 1998 hadi 2017 amewasili nchini
kuonana na viongozi wakuu wa serikali, nini maoni yako kuhusu hili?
JIBU Sisi
hatukushughulika na uchimbaji wa madini, lakini utafiti tulifanya na
kujua madini yapo na kuna maeneo mengi ambayo tumeweza kufanya vizuri
tunapata mapato, lakini hatukupata mapato yote.
Lakini
hili la mchanga sitaki kulizungumzia sana nadhani watu wanalichukulia
kwa mihemko sioni faida kuzungumzia matukio badala ya kuona tafsiri
nzima nini cha kufanya.
Ninachokiona
na cha muhimu sana, Watanzania wamepata faida kwa mara ya kwanza
tumeweza kujua mikataba ya madini ikipitiwa na Kamati zote mbili
zimetueleza maeneo yote ya mikataba waliyopitia na kuja na mapendekezo.
Tumetambua serikali ilikuwa na hisa au la mrahaba asilimia ngapi, kodi
kiasi gani, na mambo kama hayo.
Naomba
jambo hili lisibague, tunasema hatupati mapato ya kutosha ni lazima
tujue kwa wachimbaji wa nje na wa ndani mfano nani anajua wachimbaji
wadogo wadogo wamechimba madini kiasi gani tangu 1998 hadi 2017 na kodi
kiasi gani imeimngia. Tumepata nafasi sasa ya kuangalia sera za kulinda
rasilimali ya madini na nyingine zote katika nchi, kama maliasili ya
bahari tunaitumiaje, gesi, makaa ya mawe, chuma, wanyama pori na mambo
kama hayo.
Hii
imetufungua macho sera ya aina gani sheria za aina gani, jinsi gani ya
kutunza na kutumia rasilimali hizi tulizopewa na mungu.
SWALI: Kwa
kuwa wananchi tulio wengi tunaenda kwa mihemko bila kupambanua hoja
husika na kutoa mapendekezo au maoni yatakayo isaidia serikali kuboresha
sera sheria na utendaji wa rasilimali zetu unadhani tatizo ni nini?
JIBU: Hatujaona
uongozi wa Kitaifa katika hili suala la mchanga wa makinikia
ninachokiona mimi ni uongozi wa chama na siasa nyingi, sio sahihi kabisa
wanafanya makosa hili ni suala la rasilimali za nchi ni la kila
Mtanzania.
Viongozi
hawawatendei haki wananchi wanaowakilisha, wanakuwa na mihemko wanasema
kamata, shitaki, wafunge. masuala ya kitaifa hayaendi hivyo sisi sio
Polisi wala Mahakama waachieni wenye kazi yao.
Uongozi
wa kulalamika hautusaidii, wananchi wanataka kuona rasilimali zetu
zinanufaisha na kuboresha huduma za jamii ambazo wanalalamika kila leo
hakuna dawa, elimu isiyowajenga vijana na mambo kama hayo.
SWALI: Mhe.
Kutokana na sakata la mchanga wa dhahabu uliokuwa unasafirishwa nje ya
nchi na matokeo yake watanzania tunajifunza nini kwa maoni yako?
JIBU: Kabla
ya tuona funzo tulilopata nadhani ni vema nikazungumzia jambo hili,
nimeona mjadala katika mitandao ya kijamii ambayo inafanywa kwa mihemko.
Ukiangalia vyombo vya habari au viongozi tumejikita katika majina ya
watu, nilikuwa nnaangalia Bunge wote wanakwenda kwa wale waliotajwa
unakuta kuna wanaochangia na wanaolaumu ama unsahangilia au unalalamika
kuhusu watu.
Kubwa
ni utaratibu tulionao haitasaidia kulalamika juu ya watu waliofanya
kazi huko nyuma, tunaweza kuwauliza wahusika nini kilitokea mpaka
kufanya hivyo, lakini hilo sio kubwa, muhimu ni kutafuta ufumbuzi.
Mjadala
huu umenikumbusha Awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere viongozi wote na
wananchi walikuwa wanalalamika kila kitu wanachokikosa ni kwa sababu ya
wakoloni. Mwalimu akasema namnukuu: “Ni kweli wakoloni wametuleta
matatizo mengi sana lakini haitoshi kulaumu wakoloni bila kuondoa mateso
ya wananchi”. Mwalimu akaja na Waraka ambao ulikuwa unaitwa “Act dont
Argue” nadhani bado upo.
Waziri
wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi nanukuu amesema.
“Napenda kupata maoni tufanye nini kuhusu suala hili la mchanga wa
dhahabu (makinikia).” Namuunga mkono, sasa tumepata nafasi ya kutoa
maoni, mawazo ambayo ni muhimu sana maoni ya wadau katika uundaji wa
sera na sheria
Sasa
hivi siamini kama hatuna utaalamu, nina hakika tunao wa kutosha tatizo
ni maadili na hilo lazima kutafuta ufumbuzi wake, pia tuunge mkono
serikali inachofanya kupambana na rushwa na ufisadi.
“Lakini
tusijidanganye bishara ya madini, mafuta ina changamoto kubwa sana
duniani hususan Afrika, maana unapambana na watu wenye fedha biashara
hii popote utakapo kwenda, ambapo uchumi unategemea mafuta na madini
utaona jinsi wakubwa wanavyooneemeka na rasilimali hizo na kuwaaacha
wananchi wakiwa masikini mfano mzuri Nigeria”.
Pamoja na kuangalia maadili na nidhamu lazima kuwe na uwazi katika mikataba ni muhimu sana.
SWALI: Una maoni na mapendekezo yako kwa viongozi wote na Mhe Rais katika kumuunga mkono?
JIBU:
Kwanza naliona hili la malumbano yatatugawa, waache tofauti zao hii
lawama ya madini ingekuwa ni mwanzo kwa kuleta mawazo na maoni ya
kutengeneza nchi yetu katika kulinda na kuzitumia rasilimali zote kwa
maendeleo ya taifa letu.
Viongozi
msaidieni Rais kulishughulikia kwa pamoja hili si jambo la chama wala
Taasisi. Hakuna haja ya kupeana lawama ukishasema tumekosea unatakiwa
ueleze tufanye nini, sio kusema serikali ichukue hatua kwani serikali ni
nani si mimi na wewe sasa kwa nini hutaki wewe kulitolea maoni?
Tujiamini
nimeona katika malumbano hayo, wengine wanaonekana kama hatujiami kama
tukifanya hivi tunaweza kushitakiwa, mabadiliko yoyote yana machungu
yake. Tusije tukapoteza imani tuliyonayo maana tunaweza tukapoteza
mapato yetu lakini ni lazima tufanye kwa kujenga afya ya rasilimali
zetu.
Rais
amekutana na mmiliki wa Barick na kila upande una msimamo wake,
tuiachie serikali na nina imani kabisa serikali itafanikiwa.
Kinachonishangaza ni mazungumzo ya baadhi ya viongozi kuwa serikali
ihakikishe tunapata hizo fedha walizo taja kwenye taarifa.
Nadhani
hii sio sahihi, tuna imani na Viongozi wet wakuu haswa Rais, lolote
litakaloafikiwa tulipokee na kulikubali tusije kuanza kulumbana ripoti
imesema trilioni 108 ziko wapi? Pia nilisemee hili la dalili za
kupoteza imani, eti tukifanya hivyo tutashitakiwa, sababu ya mikataba
na wawekezaji hawatakuja mimi naamini watakuja tu rasilimali zipo kwetu
hawana jinsi.
SWALI: Msaada wako binafsi kwa Rais au maoni yako kwa Rais
JIBU:
Sisi tupo, Uongozi ni suala la kupeana vijiti mimi natoka Mara
nimepitia utamaduni wa kabila langu kwa utamaduni wetu unafika mahali
unangatuka watu wanadhani kungatuka ni kustaafu hapana sio sahihi.
Ukitoka jandoni mzee wako lazima angatuke maana umekuwa sehemu ya jeshi
la kabila na yeyote ambaye kijana wake yuko kwenye jeshi yeye anatoka.
Wazee
hawaingii katika mambo ya vijana na sisi tupo lakini hatutaki kuingilia
utendaji wao kama sisi tulivyoachiwa kuendesha nchi, ila Rais
akituhitaji tupo tayari kwa ajili ya ushauri anaweza kuukubali au
kuukataa. Nataka nimhakikishie kwa hili tupo pamoja na tutatoa maoni ya
kurutubisha Sera, Sheria na Utendaji katika rasilimali za nchi hii.
0 comments:
Chapisha Maoni