MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema Tanzania inapaswa
kuhakikisha sheria na sera za madini zinalazimisha rasilimali madini
kuwa mali ya Watanzania ndipo nchini itanufaika.
Aidha, amesema ni wakati muafaka kwa Taifa kujitoa katika mfumo wa kodi
za Kimataifa akiuelezea kuwa umeonesha kunyonya nchi maskini zaidi na
kunufaisha zile tajiri.
Zitto alisema hayo jana wakati akizungumza kwenye kipindi cha Mizani ya Wiki kinachorushwa na televisheni ya Azam Dar es Salaam.
Alisema kwa kuwa Rais John Magufuli ameamua kupigania vita hiyo ni
jukumu la kila Mtanzania kupigana hadi kuhakikisha kuwa madini yanakuwa
ni mali ya wananchi wa Kitanzania.
Zitto alisema kwa mujibu wa sheria iliyopo inaanisha kuwa baada ya
mwekezaji kuingia mkataba na Serikali madini ni mali yake jambo ambalo
halikubaliki.
“Hii vita ni vita ngumu ila kwa sababu Rais ameamua kuipigana pamoja na
ukweli kuwa anajua jitihada za Serikali iliyopita tunapaswa kumuunga
mkono ili tuweze kunufaika.
“Mimi nataka mambo haya mawili yaangaliwe ili kuhakikisha kuwa
rasilimali madini inatambulika kama mali yetu kwani kwa sasa ni mali ya
mwekezaji,” alisema.
Alisema iwapo sheria inapaswa kumtambua mwekezaji kama mkandarasi kwani kwa sasa inamfanya aonekane ndiye mwenye mali.
Mbunge huyo alisema kwa mujibu ya sheria ya gesi na mafuta mwekezaji ni
mkandarasi ambapo akipata bidhaa husika anarejesha gharama yane na
katika faida nchi inagawana na mwekezaji kwa sawa au nchi kupata zaidi.
Alisema jambo la pili ni mfumo wa kodi wa kidunia umeweka mazingira
ambayo kampuni za Kimataifa zinauwezo wa kuhamisha mapato yake kwenda
kwenye visiwa ambavyo kodi zipo chini hali ambayo inachangia wasilipe
kodi.
Mbunge huyo alisema mfano mwaka 2011 Kampuni ya Barick wakati huo ambayo
kwa sasa ni Acacia ilitoa taarifa ya kupata hasara nchini ila ilionesha
kupata faida nchini Uingereza hivyo kulipa kodi kwa Malkia.
Zitto alisema katika kukabiliana na hali hiyo dunia ilianza mjadala wa
kuhakikisha kuwa kodi hizo zinapatikana na Tanzania ilikuwa ni
mwenyekiti wa mjadala huo ila tangu Serikali ya awamu ya tano iingie
madarakani imeonekana kuachwa.
“Ni masikitiko makubwa kwa Serikali ya Tanzania kuacha mjadala ambao
tulikuwa tunaongoza wa mfumo wa kodi za Kimataifa ambao ungeweza
kutuletea mabadiliko chanya ya rasilimali madini ambayo inaonekana haina
faida kwa nchi na wananchi,” alisema.
Mbunge huyo alisema tipoti ya Profesa Abdulkarim Mruma haina jipya
katika ripoti ya Jaji mstafufu Mark Boman ambayo ilianisha yote
yaliyoanishwa kwa sasa.
Zitto alisema kamati hiyo ilipendekeza miaka tisa iliyopita kuwepon kwa
mashine ya uchenjuaji inakuwepo ikiwa ni pamoja na kuwepo sera na sheria
sahihi kwa sekta hiyo.
“Nakumbuka nilikuwa masomoni nchini Ujerumani nilirudi kupitisha sheria
hiyo ambayo ilipangiwa kutumia wiki moja ila muda haukutosha ikawa wiki
mbili na tulishirikisha watu asasi za kiraia ili kutusaidia kupata
mkuafaka,” alisema.
Mbunge huyo alisema kwa ushirikiano huo ilikuwa rahisi wajumbe wa kamati
ya Bunge ya Nishati na Madini kufanya kazi na kuja na mapendekezo
sahihi kuhusu rasilimali hiyo.
Alisema wao kama chama wamejipanga kufanya mjadala mwisho wa wiki hii
kuhakikisha jamii inatambua rasilimali madini kwa undani ili kila mtu
aweze kufahamu kila kitu.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Dk. Benson Bana alisema ni wakati muafaka wa Watanzania
kujitathmini kuwa wana matatizo gani.
Alisema ni vema kuangalia uwezekano wa kutumia wataalam mbalimbali
duniani kuhusu rasilimali zake ili ziweze kunufaisha jamii kwa ujumla.
Bana alisema ukifuatilia mfumo wa kutunga sera na sheria za nchi
unaonekana kufuata misingi nataratibu zinazohitajika ila kumekuwepo na
changamoto ya usimamizi na utekelezaji.
“Wakati mwingine najiuliza tunakwama wapi ila nabakia na tafsiri mbili
kwamba kuna mashinikizo ya wazi na yasiyo ya wazi hivyo tunapaswa
kujipanga kukabiliana na hali hiyo,” alisema.
0 comments:
Chapisha Maoni