Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa
magari mapya matatu ya kubebea wagonjwa kwa Wabunge watatu wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuwasaidia wananchi wa maeneo yao ya
ubunge.
Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amekabidhi magari hayo aina ya Land
Cruiser Hardtop kwa niaba ya Rais Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Mbunge
wa Nkasi Kaskazini Mkoa wa Rukwa Mhe. Ally Keissy, Mbunge wa Viti Maalum
Mkoa waTabora Mhe. Munde Tambwe na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa
Shinyanga Mhe. Lucy Mayenga.
Akizungumza
baada ya makabidhiano hayo, Balozi Kijazi amesema Mhe. Rais Magufuli
ametoa magari hayo baada ya kuguswa na kilio cha muda mrefu cha Wabunge
hao waliokuwa wakiomba wananchi wao wapatiwe magari ya wagonjwa.
“Mhe.
Rais ameamua kuwakabidhi nyinyi haya magari kutokana na vilio vyenu
ambavyo amekuwa akivisikia mara kwa mara, Mhe. Keissy umekuwa hata
ukitafuta miadi ya kuja kumuona Mhe. Rais kwa suala hili, Waheshimiwa
Wabunge wamekuwa wakiyazungumza haya kwa muda mrefu.
“Tunafahamu
kila Mbunge katika jimbo lake anahitaji kupata huduma kama hii, na
huduma kama hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,
kwa hiyo sisi Serikali kila tunapopata uwezo basi tunasaidia pale
tunapoweza kufikia kwa wakati ule, tulishatoa magari mengine matatu kama
haya Chalinze na vituo vingine vya Morogoro.” Amesema Balozi Kijazi
Balozi
Kijazi amewapongeza Wabunge hao kwa kupata magari hayo kwa ajili ya
wananchi wao na amewasihi kuhakikisha yanatunzwa vizuri ili yadumu muda
mrefu na yawahudumie wananchi wote bila kujali dini, kabila, itikadi zao
za kisiasa wala makundi.
Kwa
upande wao Mhe. Ally Keissy, Mhe. Munde Tambwe na Mhe. Lucy Mayenga
wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuitikia kilio chao cha kuwasaidia
wananchi magari ya kubebea wagonjwa, na wamempongeza kwa kazi nzuri ya
kuwapigania Watanzania wote hasa wenye shida na pia kwa juhudi kubwa za
kuleta maendeleo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
09 Mei, 2017
Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi (kati) akiwa na Katibu Mkuu Ikulu Mhe.
Alphayo Kidata (Kushoto) na Mkurugenzi wa Huduma Ikulu Bw. Charles
Mwankupili (kulia) na Wabunge Mhe Ali Mohamed Kessy (mbunge wa Nkasi
Kaskazini) Mhe. Munde tambwe na Mhe Lucy Mayenga (wabunge viti
maalumu) baada ya kuwakabidhi magari la kubebea wagonjwa waliyopewa
msaada na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam leo Mei 9, 2017.