Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema
Serikali inatarajia kuandaa sheria itakayowabana madalali katika sekta
ya ardhi.
Amesema
lengo la sheria hiyo ni kuwabana madalali hao ambao wamekuwa wakiuza
ardhi katika siku za mapumziko kutokana na sababu wanazozijua wao.
Lukuvi aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18.
“Wizara
hii itatunga sheria ya kuwadhibiti madalali wanaowaonea wananchi kwa
kuuza nyumba siku za sikukuu na weekend. Hao kiama chao kinakuja kwa
sababu tutawatungia sheria na tutawatambua kwa sifa zao kisheria.
“Hata wenye maeneo makubwa mijini, lazima tutaanza kuwatambua na kuwatoza kodi hata kama hawajayapima.
“Utakuta
mtu anamiliki ekari 30 mjini, zote hizo za nini, utafika wakati
tutawazuia kuuza maeneo hayo kwa sababu wanaiibia Serikali,” alisema
Lukuvi.
“Katika
hilo, Serikali imejipanga kuhakikisha kila ardhi iliyopo nchini,
inapimwa na kutumika kwa usawa na haki kama ilivyokusudiwa kwani kuna
watu wanatakatisha fedha zao kupitia sekta ya ardhi,” alisema Lukuvi.
Kuhusu
utoaji wa miliki za ardhi, alisema wizara yake itaendelea kushirikiana
na halmashauri na sekta binafsi kuhakikisha kila ardhi inapimwa na
kumilikishwa.
“Katika
mwaka wa fedha 2016/17, wizara iliahidi kuandaa hatimiliki za ardhi
400,000 na kutoa hati za hakimiliki za kimila 57,000.
“Hadi
kufikia Mei 15 mwaka huu, wizara imetoa hatimiliki za ardhi 33,979 na
imeratibu uandaaji wa hati za hakimiliki za kimila 35,002 na pia wizara
imeandaa vyeti vya ardhi za viijiji 505.
“Lakini,
katika mwaka wa fedha 2017/18, wizara yangu kwa kushirikiana na
halmashauri nchini, itaandaa hatimiliki za ardhi 400,000, vyeti vya
ardhi ya vijiji 1,000 na kutoa hati za hakimiliki za kimila 57,000.
“Ili
kuwawezesha wananchi wengi kupata hatimiliki za ardhi, wizara
inakusudia kupunguza tozo ya mbele ambayo hutozwa wakati wa kumilikisha
kutoka asiliia 7.5 mpaka asilimia 2.5 ya thamani ya ardhi.
“Kwa
hiyo, natoa wito kwa halmashauri zote nchini, kuhakikisha zinamilikisha
viwanja vyote vilivyopimwa na kuandaa hati ili wananchi waweze kuwa na
miliki salama,” alisema Lukuvi.
Wakati
huo huo, alisema wizara yake itaendelea kuhakiki viwanja na mashamba
nchini ili kubaini ukiukwaji wa masharti ya umiliki .
Pamoja
na hayo, alisema baada ya kufanya uhakiki siku zilizopita, wizara yake
imeshabatilisha miliki za viwanja 227 na mashamba 17 kutokana na
ukiukwaji wa masharti. Viwanja na mashamba hayo, viko katika Mikoa ya
Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Iringa, Kagera na Morogoro.
Naye
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alimtaka Waziri Lukuvi
atakapoanza kuchukua hatua kwa waliokiuka sheria za ardhi, asiangalie
itikadi za kisiasa na badala yake kila mmoja achukuliwe hatua kwa mujibu
wa sheria.
Kuhusu
mradi wa viwanja 20, 000 jijini Dar es Salaam, aliitaka Serikali ifanye
uhakiki wa viwanja hivyo ili kujua uhalali wa viwanja hivyo.
Pia,
alitaka sheria za kimila za umiliki wa ardhi zinazowakandamiza
wanawake, alitaka ziangaliwe upya ili wanawake nao wawe na haki ya
kumiliki ardhi kama walivyo wanaume.
Naye
Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM), alitaka migogoro ya
ardhi inayohusisha wananchi na maeneo ya jeshi, itatuliwe haraka ili
wananchi waishi kwa amani.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma (CUF),
alilalamikia bei ya nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kusema
zinauzwa kwa bei kubwa ingawa viongozi wa shirika hilo wamekuwa
wakisema zinauzwa kwa bei ndogo.
0 comments:
Chapisha Maoni